Mawaziri wa mambo ya nje wa G20 wakutana Brazil
21 Februari 2024Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wapo mjini Rio de Janeiro kuhudhuria mkutano huo wa kwanza wa ngazi ya juu wa G20 mwaka huu.
Mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi hatohudhuria. Brazil, ambayo ilichukua urais wa kupokezana wa G20 kutoka kwa India Desemba mwaka jana, imeelezea matumaini ya kile Rais Luiz Inacio Lula da Silva anachokiita "jukwaa lenye uwezo mkubwa zaidi wa kushawishi ajenda ya kimataifa kwa njia chanya."
Lakini mwishoni mwa wiki akiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika, Lula alianzisha mgogoro wa kidiplomasia kwa kuituhumu Israel kuwa inafanya "mauaji ya halaiki", akiilinganisha operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza na maangamizi yaliyofanywa dhidi Wayahudi.