Mawaziri wa mambo ya kigeni wa ASEAN wakutana Laos
24 Julai 2024Nchi za jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN, zimekutana hivi leo mjini Viantiene nchini Laos huku zikipania kuendeleza juhudi za kuutanzua mgogoro nchini Myanmarna kutuliza wasiwasi kuhusu suala la bahari ya China Kusini.
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo watajadili mkwamo katika juhudi za kuufikisha mwisho mgogoro ambao umegeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar ambao Umoja wa Mataifa unasema imewalazimu watu milioni 2.6 kuyakimbia makazi yao.
Wanachama wakubwa wa jumuiya ya ASEAN zikiwemo Thailand, Indonesia, Singapore na Malaysia zimekatishwa tamaa na hatua ya utawala wa kijeshi kutokuwa tayari kutimiza ahadi zake kufanya mdahalo, hali ambayo imeiweka katika mtihani uaminifu na uwezo wa jumuiya hiyo kutekeleza mpango wa amani uliokubaliwa miezi kadhaa baada ya mapinduzi ya mwaka 2021.
Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje utafuatiwa na mikutano miwili ya kilele mjini Laos siku ya Jumamosi inayolenga kushughulikia masuala ya kimataifa, utakaohudhuriwa na maafisa kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Japan, China, urusi na kwingineko.