1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa kigeni wa NATO wakutana Jamhuri ya Czech

30 Mei 2024

Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa NATO wanakutana jamhuri ya Czech leo katikati ya miito ya kuyataka mataifa washirika kuondoa vizuizi vinavyoikataza Ukraine kutumia silaha za mataifa ya magharibi kushambulia Urusi.

https://p.dw.com/p/4gS05
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akiwa na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akiwa na Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Mkutano huo wa siku mbili kwenye mji mkúu Prague, unanuwia kupigia upatu mpango wa kutangaza msaada zaidi kwa Ukraine wakati wa mkutano wa kilele wa NATO utakaofanyika mjini Washington, Marekani hapo mwezi Julai.

Hata hivyo ajenda ya iwapo Ukraine ipatiwe ruhusa ya kutumia silaha zilizotolewa na nchi za magharibi kuyalenga maeneo ndani ya Urusi yumkini itatawala mkutano huo wa mjini Prague.

Soma pia:Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya washindwa kufikia makubaliano kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za mataifa hayo katika ardhi ya Urusi

Kwa miezi kadhaa sasa, Ukraine imekuwa ikiwashinikiza washirika wake -- hasa Marekani -- kuiruhusu itumie silaha za masafa marefu inazopokea, kuishambulia Urusi.

Hadi sasa Marekani na Ujerumani zimekataa kutoa idhini hiyo zikihofia inaweza kuzitumbukiza kwenye mzozo wa kijeshi na Moscow.