Hali bado ni tete
1 Julai 2015Mawaziri wa fedha wa nchi za kanda ya sarafu ya euro wataendelea na mazungumzo kuhusu mgogoro wa Ugiriki hapo baadae Jumatano, kuliko ilivyokuwa imepangwa awali, ikiwa ni baada ya kulikataa pendekezo la nchi hiyo kutaka msaada wa fedha wa miaka miwili. Wakati hali inazidi kuwa tete, Mkuu wa kundi hilo Jeroen Dijssebloem amesema mazungumzo hayo sasa yatafanyika Jumatano jioni badala ya asubuhi. Mawaziri hao watalijadili zaidi pendekezo la Ugiriki kutaka paweko na mpango mpya wa kuiokoa isifilisike, ili kunusuru kuisukuma zaidi katika uwezekano wa kujitoa kwenye kanda hiyo ya sarafu ya euro.Mazungumzo ya leo yatafanyika siku moja baada ya Ugiriki kushindwa kutimiza wajibu wake wa kulilipa Shirika la Fedha la Kimataifa –IMF deni la euro bilioni 1.5 hapo jana , na kuwa nchi ya kwanza ya kiviwanda kufilisika na kushindwa kulilipa Shirika hilo.Kwa mujibu wa Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras, nchi yake imeomba msaada zaidi wa euro bilioni 29.1 kutoka mfuko maalum unaojulikana kama mfuko wa utulivu wa fedha wa Ulaya, ili iweze kukidhi kikamilifu mahitaji yake ya fedha na kushajiisha madeni kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.
Maafisa wa Ugiriki wamedokeza kwamba watakuwa tayari kusitisha kura ya maoni kuhusu mageuzi yanayotakiwa na wakopeshaji -kura ambayo inatarajiwa kufanyika Jumapili, ikiwa mazungumzo ya leo hatimae yatafanikiwa kuleta makubaliano ya dakika ya mwisho kuhusu pendekezo la Ugiriki kutaka ufadhili mpya kwa kipindi cha mika hiyo miwili.Waziri wa fedha Yanis Varoufakis aliwaambia mawaziri wenzake kwamba chama tawala SYRIZA kitakuwa tayari hata kuwataka Wagiriki kupiga kura ya”ndio” Jumapili, ikiwa nchi yake itapatiwa mkopo mpya.
Kungali na hali ya ati ati miongoni mwa washirika wa Ugiriki. Nchini Ujerumani, mkopeshaji mkubwa wa Ugiriki, mbunge Hans Michelbach kutoka chama cha Christian Social Union, mshirika wa kundi la wahafidhina la Kansela Angela Merkel, ameishutumu Ugiriki kwa kile alichosema ni kuipotosha Ulaya na kusema itakuwa kosa kuipa mkopo mpya. Kwa upande mwengine Waziri wa fedha wa Ufaransa Michel Sapin ambaye amekuwa mwenye kuzingatia sana kilio cha Ugiriki miongoni mwa nchi za kanda ya euro, ameiambia redio ya RTL kwamba lengo ni kupata makubaliano kabla ya kura ya maoni kama itawezekana, lakini hali inatatanisha.
Utafiti wa maoni ya wapiga kura leo, umeonyesha kambi ya wanaoyapinga mageuzi hayo ya kiuchumi inaongoza ikiwa ni baada ya waziri mkuu Tsipras kuukataa mpango wa mageuzi hayo uliopendekezwa na wakopeshaji-Umoja wa Ulaya, Benki kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, akiuita ni wenye kudhalilisha. Lakini kwa upande mwengine inaelekea uongozi wa kura ya”hapana” unapunguwa, baada ya serikali kulazimika kuzifunga benki na kuweka ukaguzi wa fedha.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, rtr,afp
Mhariri: Iddi Ssessanga