1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLuxembourg

Mawaziri wa EU wasaka masuluhisho ya migogoro ya kikanda

23 Oktoba 2023

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wasaka muafaka wa njia ya kuchukuwa kusaidia kutatua mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4XuzL
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akiwasili Luxembourg kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Oktoba 23, 2023.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akiwasili Luxembourg kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Oktoba 23, 2023.Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Mawaziri hao pia wanajadili jinsi ya kuifadhili Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi ambao unaelekea kuingia msimu wa pili wa majira ya baridi. 

Josep Borrell, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, amesema wito wa usitishaji vita katika Ukanda wa Ghuba uliotolewa na Umoja wa Mataifa ni kati ya ajenda zinazojadiliwa na mawaziri hao wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya.

Wito huo unaungwa mkono na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya ikiwemo Uhispania, Ireland na Uholanzi. Lakini nchi nyingine kama Ujerumani na Austria zinapinga mwelekeo huo, zikisisitiza haki ya Israel kujilinda. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock amesema:

"Kwa Ujerumani, ni wazi kwamba Waisraeli na Wapalestina wanaweza kuishi kwa amani ya kudumu na kwa usalama, ikiwa hakutakuwa na ugaidi na mateso ya binadamu na suluhisho la mataifa mawili.”

Lori ambayo ni sehemu ya msafara unaoelekea Gaza kupeleka misaada ya kibinadamu. Oktoba 22, 2023.
Lori ambayo ni sehemu ya msafara unaoelekea Gaza kupeleka misaada ya kibinadamu. Oktoba 22, 2023.Picha: Ahmed Gomaa/Xinhua/IMAGO

Wito wa kutokomeza ugaidi na kuruhusu misaada Gaza

Baerbock ameongeza kuwa haiwezekani kudhibiti mgogoro wa kibinadamu ikiwa ugaidi utaendelea jinsi ulivyo mjini Gaza. Akiashiria kuwa muda umewadia kwa Hamas kuacha kuchochea hali hiyo tete kuwa mbaya zaidi.

Lakini kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Micheal Martin, amesema usitishaji mapigano ni haja ya dharura sana ili kuruhusu misaada ya kibinaadamu, zikiwemo dawa, kupelekwa Gaza. Martin amesisitiza kuwa vifo ni vingi na ni sharti vikomeshwe.

Kulingana na Martin, mateso ya raia, hususan watoto, ni katika viwango vinavyohitaji usitishaji vita mara moja.

Miongoni mwa ajenda kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ni jinsi ya kuzuia kutanuka kwa migogoro ya kikanda.
Miongoni mwa ajenda kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ni jinsi ya kuzuia kutanuka kwa migogoro ya kikanda.Picha: Alexandros Michailidis/European Union

Borrell vile vile alisisitiza umuhimu wa kuruhusu misaada kupelekwa Ukanda wa Gaza.

Juhudi za kuzuia mizozo kutanuka

Swali la jinsi Umoja wa Ulaya unavyoweza kuzuia migogoro ya kikanda kutanuka zaidi pia linajadiliwa, ukiwemo mgogoro wa Ukraine na Urusi, halikadhalika Azerbaijan na Armenia.

Kuhusu Ukraine, wajumbe hao watahitajika kufafanua bayana katika miezi ijayo jinsi Umoja wa Ulaya utakavyopaswa kutekeleza mipango ya ahadi za kiusalama ambazo zimewekwa na nchi za Magharibi.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amependekeza ufadhili wa muda mrefu wa misaada ya kijeshi na pia kutumia fedha za Umoja wa Ulaya kusaidia katika kununua ndege za kivita za kisasa pamoja na makombora.

Hususan anataka kiasi cha dola bilioni 5.3 kutolewa kila mwaka kuanzia mwaka 2024 hadi mwisho wa mwaka 2027.

(Vyanzo: DPAE, APTN)