1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa EU kujadili uwezekano wa vikwazo zaidi kwa Syria

17 Oktoba 2016

Vikwazo hivyo huenda vikajumuisha marufuku ya usafiri na kuzuiwa kwa mali za wakuu wa kisiasa na kijeshi

https://p.dw.com/p/2RIwd
Luxemburg Steinmeier beim EU Außenministertreffen
Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya Umoja wa Ulaya wanaokutana nchini Luxembourg wanajadili uwezekano wa kuongeza vikwazo zaidi dhidi ya Syria kufuatia kuyumba kwa juhudi za kuzuia mashambulizi dhidi ya mji Aleppo vita na kuwapatia raia misaada, ingawa hakuna nchi yoyote ya Umoja wa Ulaya iliyopendekeza Urusi kuwekewa vikwazo licha ya kumsaidia Rais Bashar al-Assad katika kushambulia mji wa Aleppo.

Vikwazo hivyo huenda vikajumuisha marufuku ya usafiri na kuzuiwa kwa mali za wakuu wa kisiasa na kijeshi wa utawala wa Assad. Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema ushahidi pia utakusanywa kwa uwezekano wa kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, dhidi ya washukiwa wa uhalifu wa kivita.

Mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, amesema huenda mawaziri hao wakaongeza Wasyria zaidi kwenye orodha ya wanaowekewa vikwazo kwa kuchangia katika ukiukaji wa haki za kibinadamu au kuchangia katika uhalifu wa kivita. Amesema "Umoja wa Ulaya si mshiriki wa kivita nchini Syria. Mimi binafsi nina fahari ya kutokuwa mmoja wao. Lakini lazima tuhamasishe na tuunge mkono juhudi zote zitakazofanikisha usitishwaji uhasama, vita na suluhisho miongoni mwa wanaohusika moja kwa moja kwenye mapigano hayo. Jinsi tu tulivyojitolea kushiriki vita dhidi ya Daesh, Dola la Kiislamu, IS, ndiyo sababu pia tuna imani kuwa juhudi za mustakabali wa kisiasa nchini Syria zitakuwa za manufaa katika vita dhidi ya Daesh."

Wanajeshi ya Syria wakifyatua makombora dhidi ya IS katika kijiji cha Yahmoul
Wanajeshi ya Syria wakifyatua makombora dhidi ya IS katika kijiji cha Yahmoul Picha: Getty Images/AFP/N. Al-Kathib

Mazungumzo kati ya Urusi na Marekani kwa ushirikiano na mataifa mengine ya Magharibi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, yalikosa kuzaa matunda yoyote yanayoweza kusitisha vita na au kuruhusu usafirishaji wa misaada kwa raia mjini Aleppo.

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amechelea kuunga mkono matumizi ya vikwazo kama njia ya kupata suluhisho la haraka nchini Syria: "Kubwa zaidi ni kwamba mazungumzo yameanza na Urusi, Marekani, Uturuki na mataifa mengne ya ghuba yanashiriki na muendelezo wa mazungumzo hayo nchini Uswizi kunaonesha matumaini ya kufaulu. Tuna deni la kufaulu kwa watu wa mashariki ya Aleppo ambao kwa wiki kadhaa hawajapata misaada ya kibinadamu."

Syrien Aleppo Bergung Opfer Luftangriff
Picha: picture-alliance/AA/I. Ebu Leys

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson, amesema mawaziri wanaokutana Luxembourg watajadili pia mbinu za kuzishinikiza Syria, Urusi na Iran kusitisha mapigano, huku akirejelea msimamo wake kuwa kuwa usitishwaji wa vita hivyo upo mikononi mwa utawala wa Assad na Urusi.

Naye, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, aliyefananisha mashambulizi dhidi ya Aleppo kuwa sawa na uliofanywa na Urusi jijini Grozny katika jimbo la Chechnia kati ya mwaka 1999-2000, amesema juhudi za kidiplomasia zimezuiliwa, na kwamba Urusi imejiingiza kabisa katika uharibifu huo ikishirikiana na utawala wa Assad.

Ayrault amesisitiza kuwa linalofanyika Aleppo ni janga la kibinadamu na ni sharti kila kinachowezekana kifanywe ili kusitisha mashambulizi ya mabomu na kuruhusu utoaji wa misaada wa kibinadamu.

Mwandishi: John Juma/APE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef