1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mawaziri wa ASEAN wadhamiria kuutatua mzozo wa Myanmar

27 Oktoba 2022

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya Kusini mashariki mwa Asia ASEAN wanakutana leo mjini Jakarta nchini Indonesia kuujadili mzozo wa kisiasa nchini Myanmar, huku wakisema wamedhamiria kwa dhati kupata suluhu.

https://p.dw.com/p/4IkMv
Indonesien | ASEAN Dringlichkeitssitzung zu Myanmar
Picha: Galih Pradipta/AP Photo/picture alliance

Myanmar imekuwa katika machafuko tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Februari mwaka jana, lakini pamoja na hali ya kutia wasiwasi, juhudi za Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) bado hazijazaa matunda yoyote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cambodia Prak Sokhonn amesema baada ya mkutano wa dharura katika sekretarieti ya umoja huo mjini Jakarta, kuwa Jumuiya ya ASEAN haipaswi kukatishwa tamaa bali idhamirie zaidi kuisaidia Myanmar kufikia suluhu ya amani.   

Soma zaidi: Mjumbe wa UN kwa Myanmar azungumza na kiongozi wa kijeshi    

Utawala wa kijeshi wa Myanmar ulikataa ombi la kutuma muwakilishi huru na asiye na uhusiano wa kisiasa kwenye mkutano huo. Kulingana na mfuatiliaji wa eneo hilo, zaidi ya watu 2,300 wameuawa katika operesheni ya kikatili ya jeshi la Myanmar dhidi ya wapinzani baada ya mapinduzi ya Februari mosi 2021. Katika mkutano huo wa Alhamisi, Marekani imehimiza kuchukuliwa hatua kali.

Wasiwasi wa Marekani kwa ufanisi wa ASEAN

Daniel Kritenbrink
Daniel Kritenbrink, Mwanadiplomasia wa Marekani katika eneo la Asia MasharikiPicha: Hoang Dinh Nam/AFP/Getty Images

Daniel Kritenbrink, mwanadiplomasia mkuu wa Marekani katika eneo la Asia Mashariki, alisema katika hafla moja huko Washington kwamba serikali ya kijeshi inadiriki kile alichokiita "uharibifu kamili wa maendeleo yote yaliyopatikana katika muongo uliopita" wakati Myanmar ilikuwa ikielekea kwenye demokrasia.

Soma zaidi: Myanmar yamkamata balozi wa zamani wa Uingereza

Kritenbrink ameendelea kusema kuwa Marekani haitakaa kimya wakati vurugu hizi zikiendelea,  huku serikali ya Myanmar ikijiandaa kwa uchaguzi ambao afisa huyo amesema utakuwa wa uongo na udanganyifu.

Aidha, Kritenbrink amebaini kuwa Washington ina "heshima kubwa" kwa Jumuiya ya ASEAN, lakini maafisa wa Marekani wameelezea kusikitishwa hapo awali kutokana na kukosekana kwa mafanikio katika mpango wa umoja huo kuhusu mgogoro huo, ambao walitaka usitishwaji wa ghasia, kuzidisha misaada na kuanzisha mazungumzo.

Kolumbien | Treffen Gustavo Petro und Antony Blinken
Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa MarekaniPicha: Guillermo Legaria/Getty Images

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken aliwahi kusema mwezi Julai kuwa anadhani nchi zote za ASEAN zinahitaji kuuwajibisha utawala wa Myanmar, na kwamba hadi sasa, hawajaona muelekeo mzuri katika hilo.

ASEAN yataja kuwa tayari kuchukua hatua

Indonesien | ASEAN Dringlichkeitssitzung zu Myanmar
Viongozi wa ASEAN wakiwa katika mkutano mjini Jakarta nchini Indonesia, 27.10.2022Picha: Galih Pradipta/AP Photo/picture alliance

Mawaziri wa ASEAN wamethibitisha tena leo Alhamisi ahadi yao kwa mpango huo wenye vipengele vitano, uliopendekezwa kwa mara ya kwanza mwezi Aprili mwaka huu, na unaohusisha usitishaji vurugu na kuanza mazungumzo ya amani.

Soma zaidi: ASEAN wakutana kujadili usalama wa kikanda

Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Myanmar Min Aung Hlaing hajaalikwa kwa mwaka wa pili mfululizo kwenye mkutano wa viongozi wa ASEAN nchini Cambodia mwezi ujao, huku Mwanadiplomasia mkuu wa Myanmar Wunna Maung Lwin akitengwa katika mazungumzo ya mawaziri wa Jumuiya hiyo ya mwezi Februari na Agosti.

Mawaziri hao wamesema wakati wa kuchukua hatua ni sasa, lakini kimsingi bado hali ni mbaya na isiyotabirika, na hii haitokani na ukosefu wa uwajibikaji wala juhudi kwa upande wa ASEAN, lakini ni kwa sababu ya utata na ugumu wa migogoro ya muda mrefu ya Myanmar.