Mawakili wa Bazoum wakanusha madai kwamba alijaribu kutoroka
21 Oktoba 2023Mawakili wa rais wa Niger aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum jana Ijumaa, walikanusha madai ya utawala mpya wa kijeshi nchini humo kwamba Bazoum alijaribu kutoroka wakati Ufaransa ikisema kwamba vikosi vyake vitakamilisha hatua ya kuondoka nchini humo kufikia mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopangwa.
Alhamisi jioni, utawala huo wa kijeshi ulisema kuwa Bazoum alijaribu kutoroka pamoja na familia yake, wapishi wawili na maafisa wawili wa usalama.
Katika taarifa kupitia televisheni ya taifa, msemaji wa utawala huo wa kijeshi Amadou Abdramane, alisema kuwa mpango huo wa kutoroka ulihusisha kuingia mafichoni viungani mwa mji mkuu Niamey kabla ya kusafiri kwa helikopta za taifa moja la kigeni lenye nguvu kueleka Nigeria.
Abdramane ameongeza kuwa mpango huo ulitibuka na wahusika kukamatwa.
Lakini kundi la mawakili wanaomtetea Bazoum ambaye yuko chini ya kizuizi cha nyumbani tangu alipoondolewa kwa nguvu madarakani mnamo mwezi Julai, wamepinga vikali madai hayo na kuyataja kuwa tuhuma za kutungwa dhidi yake.