1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya Afrika Kusini yakumbusha enzi za ukaburu

17 Agosti 2012

Polisi wenye silaha nzito wameonekana wakipiga doria katika mgodi wa madini ya Platinum nchini Afrika Kusini, ambako zaidi ya wafanyakazi 30 waliuwawa jana katika tukio linalolinganishwa na zama za ukaburu.

https://p.dw.com/p/15reK
Wafanyakazi wa machimbo ya madini wakiwa na silaha za kienyeji kujihami na mashambulizi ya polisi.
Wafanyakazi wa machimbo ya madini wakiwa na silaha za kienyeji kujihami na mashambulizi ya polisi.Picha: picture-alliance/dpa

Baada ya kimya cha maafisa wa serikali kwa zaidi ya masaa 12, Waziri wa Polisi, Nathi Mthethwa, alithibitisha kiasi ya watu 30 waliuwawa katika operesheni hiyo ya polisi iliyofanyika katika mgodi huo uliopo kiasi cha kilometa 100 kaskazini magharibi mwa Johannesburg.

Polisi waliwafyatulia risasi kiasi ya watu 3,000 walikuwa na mapanga na fimbo mikononi kwa madai ya kutotii amri yao ya kuwataka watawanyike. Mthethwa amesema idadi ya waliouwawa katika tukio hilo inaweza kuongezeka. Lakini chama cha wafanyakazi nchini humo kimisema waliouwawa ni watu 35.

Akizungumza na radio moja nchini Afrika Kusini iitwayo "Talki Radio 702", waziri huyo mwenye dhamana na usalama wa raia, amesema idadi ya watu waliojeruhiwa ni kubwa.

Serikali yawatetea polisi

Hata hivyo, alilitetea jeshi la polisi kwa kusema polisi pia walishambuliwa na wachimba madini hao, wanachama wa Chama cha Wachimbaji Madini na Ujenzi (AMCU), ambacho kimekuwa kikipingana na chama kingine kikubwa cha uchimbaji madini nchini humo, (NUM), kwa takribani miaka 25 sasa.

Polisi wakikabiliana na mashambulizi ya waandamanaji katika mgodi wa madini ya Platinum.
Polisi wakikabiliana na mashambulizi ya waandamanaji katika mgodi wa madini ya Platinum.Picha: Reuters

Waziri huyo alisema wagomaji waliwafyatulia polisi risasi kutoka katika mjumuiko wao, jambo ambalo liliwafanya polisi walipize kisasi.

Msemaji wa chama cha taifa wachimbaji madini, NUM, alisema ilikuwa ajali mbaya kabisa. "Kama mtu atakuja katika nyumba yako na kuanza kuishambulia familia unahitaji majadiliano? Huhitaji majadiliano yoyeyote bila shaka. Unahitaji hatua madhubuti kuchukuliwa na vyombo vya sheria. Amani katika eneo lolote la sekta ya madini nchini sio la kujadiliwa."

Rais Jacob Zuma amesema ameshtushwa na kupata hofu sana kufuatia mkasa huo unaotajwa kuwa ni umwagikaji mkubwa wa damu kuonekana katika operesheni za jeshi la polisi tangu kumalizika kwa utawala wa Wazungu wachache mwaka 1994.

Hali sasa ni shwari

Baada ya tukio hilo la jana, eneo la mgodi huo hivi sasa limekuwa tulivu zaidi, huku likiwa na ulinzi mkali wa polisi wenye silaha nzito nzito, yakiwemo magari na helikopta.

Wafanyakazi walio kwenye mgomo wakiimba katika mgodi wa Platinum.
Wafanyakazi walio kwenye mgomo wakiimba katika mgodi wa Platinum.Picha: Reuters

Mwanamke mmoja, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwenye vyombo vya habari aliliambia shrika la Reuters kwamba hakukuwa na vurugu zozote zilizotokea usiku wa kuamkia leo, huku akionesha kwamba tatizo lipo katika sehemu fulani ya mgodi ambayo mauwaji yalitokea jana.

Makao mkuu ya mgodi huo wa madini ya Platnium yaliyopo London, Uingereza, yamelazimika kufunga shughuli zote za uchimbaji madini ambazo zinachangia asilimia 12 ya uzalishaji wa madini hayo duniani kote. Na hisa zake zimeporomoka kwa zaidi ya asilimia 13 tangu kuanza kufukuta kwa mzozo huo wiki kadhaa zilizopita.

Afrika Kusini inafahamika duniani kote kwa kuwa na kiasi cha asilimia 80 ya hazina yote ya madini ya Platinium. Lakini kupanda kwa gharama za nishati na mishahara, na kushuka kwa bei ya madini hayo kwa mwaka huu kunafanya migodi mingi kupigania kutaka kuendelea.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Miraji Othman