Mauaji mengine ya maangamizi yahofiwa kufanyika Syria
13 Julai 2012Ikiwa taarifa za mauaji hayo zilizotolewa leo na upinzani nchini Syria zitathibitishwa, basi haya yatakuwa mauaji makubwa zaidi kuliko yale yaliyofanywa na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali katika kijiji cha Houla hapo Mei 25, ambapo watu 108 waliuawa.
Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake makuu London, Uingereza, limesema kwamba vikosi vya serikali vilitumia vifaru na helikopta kuwauwa zaidi ya watu 150 katika kijiji cha Treimsah kilicho kwenye jimbo la kati la Hama hapo jana, huku kiongozi mmoja wa waasi, Abu Mohamad, akisema idadi ya waliouawa ni 200.
Mkuu wa Shirika hilo, Rami Abdel Rahman, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba miili 30 ya wanavijiji tayari imeshatambuliwa. "Haya ni mauaji makubwa zaidi tangu kuanza kwa vuguvugu. Lazima jeshi litakuwa limepata idhini ya kufanya mauaji ya maangamizi, na Rais Assad anawajibika kwa mauaji haya." Amesema Abdel Rahman.
Serikali yavituhumu vyombo vya habari
Hata hivyo, katika taarifa yake kuhusu mauaji hayo ya Treimsah, serikali ya Syria imevituhumu vyombo vya habari ilivyoviita "vyenye kiu ya damu" na makundi ya kigaidi kuhusika nayo.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo na shirika la habari la serikali, SANA, imesema kwamba mauaji hayo yamefanywa na wale wanaotaka kujenga picha mbaya dhidi ya Syria, katika wakati ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana.
Baraza la Kitaifa la Syria, ambao ni muungano mkubwa wa upinzani nchini humo, umelitaka Baraza la Usalama kupitisha azimio la haraka dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad, kwa kutumia Sura ya Saba ya Mkataba wa Umoja huo, ambayo inaruhusu hatua kali dhidi ya utawala unaohatarisha amani ya watu wake.
Baraza la Usalama lakutana
Ripoti za mauaji hayo zimekuja baada ya mabalozi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya mazungumzo yao ya kwanza ya rasimu ya azimio juu ya Syria, ambalo linabishaniwa kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi na ambapo Urusi imekuwa ikipinga wito wa kuwekewa vikwazo zaidi kwa utawala wa Rais Assad.
Hakuna maendeleo yoyote yaliyoripotiwa kupatikana, huku muda wa mwisho uliowekwa wa tarehe 20 Julai ukikaribia. Huo ndio muda wa mwisho wa idhini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, ambako wanaharakati wanasema hadi sasa zaidi ya watu 17,000 wameshapoteza maisha yao tangu Machi 2011 mgogoro huo ulipoanza.
Wakati hayo yakiendelea, Urusi imemtaka mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan, kufanya kazi kwa karibu zaidi na upinzani. Chanzo kimoja kutoka wizara ya mambo ya nje ya Urusi kimesema kwamba nchi hiyo itashinikiza hilo katika mazungumzo kati yake na Annan hapo Jumatatu.
Ziara ya pili ya Annan nchini Urusi tangu ateuliwe kuwa mjumbe maalum kwa Syria inafuatia mkutano wa waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, na upinzani wa Syria, mapema wiki hii. Hadi sasa hajasemwa ikiwa Annan atakutana pia na Waziri Mkuu Dmitry Medvedev na Rais Vladimir Putin.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman