1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya kusitishwa mapigano Syria yafifia

16 Februari 2016

Uturuki imeishutumu Urusi kwa kufanya “uhalifu wa kivita” baada ya mashambulizi ya makombora kaskazini mwa Syria kuwauwa karibu watu 50. Mvutano huo imeyaathiri matumaini ya kutekelezwa mpango wa kuweka chini silaha

https://p.dw.com/p/1Hw0z
Syrien Aleppo Ruinen nach Bombardement Flüchtlinge
Picha: picture-alliance/AA/I. Ebu Leys

Uturuki pia imewaonya wapiganaji wa Kikurdi kuwa watachukuliwa hatua kali ikiwa watajaribu kuukamata mji mmoja karibu na mpaka wa Uturuki. Umoja wa Mataifa umesema takribani raia 50 waliuawa jana wengi wao watoto, wakati makombora yalipozipiga hospitali tano ikiwemo moja ya shirika la msaada la Madaktari wasio na Mipaka na shule mbili katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi nchini Syria, mashambulizi ambayo umoja huo umeyataja kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Aitor Zabalgogeazkoa, ni mwakilishi wa Shirika la MSF nchini Uturuki

Syrien Idlib Krankenhaus Raketenangriff
Mojawapo ya vitio vya matibabu vilivyoshambuliwaPicha: Reuters/Social Media Website

Mashambulizi ya serikali ya Syria ikisaidiwa na mabomu ya Urusi na wapiganaji wa Kishia wa Iran yameliwezesha jeshi la Syria kuukaribia mpaka wa Uturuki. Kundi la wapiganaji wa Kikurdi la YPG – ambalo Uturuki inalichukulia kuwa la kigaidi – limeitumia hali hiyo, na kutwaa udhibiti kutoka kwa waasi wa Syria na kujiimarisha katika mpaka huo.

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu ameishutumu Urusi kwa kufanya mashambulizi hayo ambayo imesema ni dhahiri huo uhalifu wa kivita. Urusi hata hivyo inasema mashambulizi hayo yaliilenga miundo mbinu ya kundi la Dola la Kiislamu. Balozi wa Syria nchini Urusi amesema ndege za Marekani ndizo zilizofanya mashambulizi hayo.

Mshauri wa Rais wa Marekani kuhusu masuala ya usalama Susan Rice alilaani mashambulizi yanayoendelea kaskazini mwa Syria, akisema yanavuruga makubaliano yaliyofikiwa wiki iliyopita na nchi zenye nguvu duniani mjini Munich. Ufaransa pia imelaani shambulizi hilo ikisema ni uhalivu wa kivita

Syrien Präsident Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/dpa/Sana

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa yuko Damascus

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amefanya ziara ya ghafla jana mjini Damascus na leo atakutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Syria. Lengo la ziara hiyo ni kuujadili mpango uliofikiwa mjini Munich wa kusitishwa mapigano kwa muda. Lakini mpango huo umetiliwa shaka na Rais Bashar al-Assad wa Syria

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ipo haja ya kuweka marufuku ya kuruka ndege katika anga za Syria ili kuwalinda raia katika maeneo ya vita. Uturuki iliyapiga ngome za Kundi la YPG kwa siku ya nne mfululizo ili kujaribu kuwazuia wapiganaji kuukamata mji wa Azaz ulioko umbali wa kilomita nane kutoka mpakani.

Waasi wa Syria, baadhi wakisaidiwa na Marekani, Uturuki na washirika wao, wanasema YPG inapigana na jeshi la Syria likisaidiwa na Urusi dhidi yao madai ambayo YPG inakanusha.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Gakuba Daniel