1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya amani yadidimia Kongo

Josephat Nyiro Charo26 Julai 2013

Uwezekano wa kupatikana mkataba wa amani mwaka huu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeonekana kila mara kuwa finyu. Mapigano mapya ya wiki iliyopita yamedidimiza zaidi matumaini.

https://p.dw.com/p/19EvX
Congolese Army soldiers man a foward position in Kanyarucinya, some 12 kms from Goma, in the east of the Democratic Republic of the Congo on July 16, 2013. The army in the Democratic Republic of Congo on July 16 pursued an offensive against rebels of the M23 movement to protect the North Kivu provincial capital of Goma. M23, a movement launched by Tutsi defectors from the army who accuse the Kinshasa government of reneging on a 2009 peace deal, last year occupied Goma for 10 days before pulling out under international pressure. AFP PHOTO / PHIL MOORE (Photo credit should read PHIL MOORE/AFP/Getty Images)
Kämpfe im OstkongoPicha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Duru mpya za mapigano katika wiki iliyopita kati ya jeshi la Kongo na kundi la waasi wa M23 yamezidi kukatisha matumaini ya kupatikana makubaliano ya aina yoyote. Kwa sasa kila upande hauonekani kuwa tayari kukubali maridhiano ya kufikiwa kwa mkataba. Lakini kuna dalili kwamba jeshi la Kongo linaanza kuwa na nguvu zaidi kuliko kundi la M23 jambo ambalo wachambuzi wanasema ni ishara ya kutia matumaini.

Msaada zaidi wa jeshi la Kongo unatoka kwa Umoja wa Mataifa, ambao unasema brigedi yake ya mapambano, ya kwanza kuwahi kupewa mamlaka ya kuyachakaza makundi ya waasi, ina wanajeshi takriban 2,000 walio tayari. Kwa sasa kiasi thuluthi mbili ya kikosi cha kimataifa kiko katika uwanja wa mapambano, amesema Madnodje Maounoubai, msemaji wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Kongo, MONUSCO.

M23 rebel soldiers keep guard during the inauguration of newly elected M23 Rebel political wing President, Bertrand Bisimwa in Bunagana on March 7, 2013. The rebel group has parted ways with their former President Bishop Jean-Marie Runiga after allegations of misuse of funds and supporting Bosco Ntaganda, a wanted war criminal. AFP PHOTO/ ISAAC KASAMANI (Photo credit should read ISAAC KASAMANI/AFP/Getty Images)
Waasi wa kundi la M23Picha: Isaac KasamaniAFP/Getty Images

Msaada wa Umoja wa Mataifa unatakiwa kuongeza kasi na uzito kwa jitihada za kuimarisha mamlaka zaidi katika maeneo ambayo kwa kiwango kikubwa yamekuwa yakidhibitiwa na waasi kwa karibu miongo miwili. Kundi la M23 lililoanzishwa mwaka 2012 na wanajeshi waasi, wengi wao wa kabila la Tutsi, limeifanya vigumu azma hiyo kufikiwa. Vikosi vyake viliuteka mji wa Goma mwezi Novemba mwaka jana. Tukio hilo la aibu la kushindwa kwa jeshi la Kongo, liliilazimu serikali ya mjini Kinshasa kushiriki mazungumzo ya kutafuta amani mjini Kampala nchini Uganda. M23 ilikuwa na furaha kushiriki mazungumzo hayo, kwa kuwa iliamini ilikuwa ikipata kutambuliwa kisiasa na kudai ilichokuwa ikikitaka ikiwa na nafasi imara kwenye mashauriano hayo.

Mambo yamebadilika

Lakini miezi kadhaa baadaye, mambo yamebadilika kabisa. Jeshi la Kongo limeimarisha uwezo wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mishahara ya wanajeshi inalipwa bila kuchelewa, na kuwapa silaha na risasi wanajeshi walio katika uwanja wa mapambano. Jeshi hilo pia limefaulu kuwahamisha wanajeshi mafisadi katika maeneo mengine yaliyo na utulivu katika taifa hilo lenye wakazi milioni 72.

Jason Stearns, mchambuzi wa masuala ya Kongo, anasema huku matatizo ya jeshi la Kongo yakiwa bado yako mbali mno kupatiwa ufumbuzi, mazungumzo na maafisa wa Umoja wa Mataifa na makamanda wa jeshi yanaashiria jeshi limekuwa imara zaidi kiasi cha kuwa kikosi bora cha mapambano vitani. Kwa mujibu wa Stearns, jeshi bado linakabiliwa na changamoto tatu kubwa zikiwemo ulezi, utapeli na kufanya makosa bila kuwa na hofu ya kuadhibiwa wala kuchukuliwa hatua yoyote kisheria.

Kwa upande mwingine mivutano ya ndani ililidhoofisha kundi la M23 na kusababisha mpasuko katika uongozi wake. Mmoja wa waasisi wa kundi hilo, Bosco Ntaganda, alipata hasara kubwa katika vita hivyo vya ndani na akalazimika kujisalimisha mwenyewe katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, mjini The Hague, Uholanzi, ambako anasubiri kesi ya mashtaka ya uhalifu wa kivita. Kwa wakati huo huo Rwanda, taifa linalotuhumiwa kwa kulisaidia kundi la M23, ilikabiliwa na vikwazo kutoka kwa mataifa ya magharibi.

Fugitive Congolese warlord Bosco Ntaganda attends rebel commander Sultani Makenga's wedding in Goma December 27, 2009. Ntaganda walked into the U.S. Embassy in Rwanda on March 18, 2013 and asked to be transferred to the International Criminal Court, where he faces war crimes charges racked up during years of rebellion. Picture taken December 27, 2009. REUTERS/Paul Harera (DEMOCRATIC REPUBLIC OF CONGO - Tags: CIVIL UNREST CRIME LAW MILITARY POLITICS SOCIETY)
Bosco Ntaganda, alipohudhuria harusi ya kamanda Sultani Makenga, Goma 27.12 2009.Picha: Reuters

Kwa sasa serikali ya mjini Kigali iko katika mtanziko, anasema Thiery Vircoulon, mchambuzi katika shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG. "Kama hawataiunga mkono M23 basi M23 itafukuzwa kutoka Kongo na jeshi la Kongo. Kama wataliunga mkono kundi hilo, watakuwa chini ya uchunguzi na huenda wakakabiliwa na vikwazo."

Mazungumzo ya Kampala shaghala bagala

Nchini Uganda, mazungumzo yamekuwa yakifanyika bila mpango, wakati wapatanishi wanapojali na kuhudhuria vikao. Daniel Bekele wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch tawi la Afrika, anasema Rwanda inabakia kuliunga mkono kundi la M23 kwa maana kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu.

Vircoulon na wachanganuzi wengine wanasema hali hii inaibua hofu kuwa kuna vivutio vichache sana kwa lengo la kuzingatia kwa bidii mazungumzo ya amani. Serikali ya Kongo inaweza pia kusita kuyakubali maridhiano kwa matumaini kwamba jeshi lake, kupitia msaada wa Umoja wa Mataifa, litaendelea kuyakomboa maeneo yanayodhibitiwa na waasi. Hadi sasa imekuwa ikiwatuma wajumbe wa ngazi ya chini katika mazungumzo ya Kampala. Hivyo, wachambuzi wanasema shinikizo jipya kutoka jeshini linapunguza uwezekano wa kuongezeka kwa machafuko, lakini halifai kwa mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman