Matumaini makubwa kwa mkutano wa London
4 Februari 2016Matarajio hayo yanatokana na kubadilika kwa mjadala wa msaada katika kipindi cha mwaka uliyopita, kufuatia mmiminikio wa mamia kwa maelfu ya wakimbizi wa Syria uliyozua tafrani katika bara la Ulaya.
Mataifa wafadhili yanayojaribu kupunguza kasi ya mmiminiko huo yatazingatia maslahi yao na vile vile kanuni za mshikamamo wa kimataifa ikiwa yatatoa zaidi ili kuboresha maisha ya wakimbizi na kuyapunguzia mzigo mataifa ya Mashariki ya Kati.
Mkutano huu umeandaliwa kwa pamoja kati ya Uingereza, Ujerumani, Norway, Kuwait na Umoja wa Mataifa. Viongozi wa dunia na wawakilishi wa mataifa kadhaa wamealikwa, sambamba na maafisa kutoka mashirika ya kimataifa, mashirika ya misaada na makundi ya kiraia.
Jumla mahitaji ya msaada yatakayowasilishwa katika mkutano huo mjini London ni karibu dola bilioni 9, yakiwemo maombi yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa kutoka kwa mashirika ya misaada ya kiasi cha dola bilioni 7.73, na maombi ya dola bilioni 1.23 kutoka serikali za kikanda zinazowahifadhi wakimbizi.
Kiwango hicho cha mwisho ni sehemu ndogo ya msaada mkubwa unaotafutwa katika miaka ijayo, na mataifa kama vile Uturuki, Lebanon na Jordan, ambayo yanawahifadhi wakimbizi wa Syria karibu milioni 4.6. Mbali na mahitaji ya msingi, wafadhili pia wanaombwa kusaidia mipango ya muda mrefu, mkazo ukiwa kwenye elimu na ajira kwa wakimbizi.
Uwekezaji, ajira, elimu ni vipaumbele
Masuala mapya ya kujadiliwa katika mktuano huo ni pamoja na mataifa wafadhili kushirikiana kwa karibu zaidi na mataifa kama Lebanon na Jordan kuimarisha chumi zao dhaifu, zinazokabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira, na kusaidia kuunda nafasi za ajira kwa raia na piawakimbizi.
Kwa sasa wakimbizi wengi wanazuwia kufanya kazi na hivyo kubakia kuwa wategemezi wa misaada haba au kulaazimika kufanya kazi zisizo rasmi na zinazowalipa pesa kidogo sana.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la kazi duniani Guy Ryder alisema ametiwa moyo kwamba mkutano wa London utayajadili mambo kwa upana wake.
"Kwa hiyo unakuwa na masuala ya kibinaadamu ambayo bado yanapewa kipaumbele, na unakuwa na mada kuhusu elimu, ambako nadhani serikali ya Norway imeweka mkazo, lakini pia una masuala ya ajira na masuala ya riziki, nadhani hii ndiyo njia sahihi, ambayo inashughulikia masuala ya kiutu, na kuyaunganisha na sehemu ya ajenda ya kimaendeleo."
Mawazo mapya pia yanhusisha uhamasishaji wa kiwango kikubwa wa kigeni katika kanda na kwa bara la Ulaya kurahisha uingizwaji katika soko lake, bidhaa zinazotengenezwa katika eneo hilo. ILO inatazamia miradi ya miundombinu inayotumia nguvu kazi kubwa, kama vile ujenzi matangi ya maji, shule na barabara. Ujerumani imependekeza kuwepo na mpango unaodhaminiwa na wafadhili wa kuzalisha ajira za muda mfupi zapatazo laki tano kwa wakimbizi walioko katika kanda hiyo.
Changamoto bado ni kubwa sana
Moja ya malengo makhsusi ya mkutano huo linashughulikia elimu - kuhakikisha watoto watoto wote wanakwenda shule katika mwaka wa masomo wa 2016/17. Kwa sasa zaidi ya watoto 700,000 wenye umri wa kwenda shule hawaendi, ambao ni zaidi ya nusu ya jumla ya watoto hao. Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa lilisema siku ya Jumanne kuwa kiasi cha dola bilioni 1.4 zitahitajika kuokoa kile kinachoweza kugeuka "kizazi kilichopotea."
Lakini licha ya nia njema na mawazo mapya, wafadhili wanakabiliwa na ukweli uliyo mchungu - mamilioni ya Wasyria wana hali mbaya zaidi kuliko walivyokuwa hata mwaka mmoja uliyopita, huku nchini Syria kwenyewe, hali ikizidi kuwa mbaya, ambapo kulingana na mashirika ya misaada, watu milioni 13.5 wanahitaji msaada.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape
Mhariri: Mohammed Khelef