1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo yakitikisa Chadema kanda ya kaskazini

29 Oktoba 2020

Eneo la mikoa ya kanda ya kaskazini ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa yanapigiwa upatu chama cha Chadema kushinda, lakini matokeo yanaonesha CCM imeibuka na ushindi, hali ambayo haikutarajiwa na wengi.

https://p.dw.com/p/3kayc
Afrika Tansania Dar es Salaam Wahlen
Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Matokeo ya ubunge na udiwani ambayo yamekwishatangazwa katika mikoa ya kanda ya kaskazini, ngome muhimu ya chama cha CHADEMA, ni pamoja na jimbo la Hai ambalo Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea kiti chake ameangushwa na mpinzani wake wa chama cha CCM Saashisa Mafuwe ambaye amepata kura 89,786 huku Mbowe akiambulia kura 27,684 kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.

Majimbo mengine ya Chadema yaliyochukuliwa na na CCM kwa kanda hii, ni pamoja na Moshi Mjini, Moshi vijijini, Hanndeni mjini, pamoja na jimbo la Arumeru Mashiriki lililokuwa mikononi mwa CCM baada ya mbunge wake aliyekuwa Chadema Joshua Nasari kufutwa ubunge na baadaye kujiunga na CCM.

Majimbo mengine ya mikoa ya Tanga na Manyara matokeo yake yanaendelea kutangazwa. Matokeo haya yamepokelewa kwa maoni mseto.

Kwa upande wa matokeo ya udiwani, jimbo la uchaguzi la moshi mjini lenye kata 21, kata 20 zimechukuliwa na CCM huku CHADEMA wakiambulia kata moja.

Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Arusha mjini Dr. John Pima, ametangaza asubuhi ya leo kwamba kata 24 kati ya 25 zimekwenda CCM huku CHADEMA wakiambulia kata moja.

Katika mkoa wa Kilimanjaro CCM imeshinda 167 Kati ya kata 169 zilizopo katika mkoa huo. Matokeo ya ubunge na udiwani bado yanaendelea kutangazwa katika maeneo mbali mbali.

Veronica Natalis DW, Arusha.

Mhariri: Zainab Aziz