1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mateka zaidi wa Israel waachiwa na kundi la Hamas

28 Novemba 2023

Israel imesema mateka wengine 11 wameachiwa huru na kundi la Hamas hapo jana usiku, ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya mkataba wa kusitisha mapigano kwa siku nne baina ya pande hizo hasimu.

https://p.dw.com/p/4ZVYK
Picha ya Abigail Edan
Picha ikimwonesha mtoto wa miaka 4 Abigail Edan, aliyechukuliwa mateka na kundi la Hamas na aliachiwa Jumapili ya Novemba 26, 2023. Picha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Kundi hilo jipya linafanya idadi jumla ya mateka walioachiwa huru tangu Ijumaa iliyopita kuwa 69 ambapo 50 ni raia wa Israel na wengine 19 kutoka mataifa mengine. Miongoni mwa walioachiwa jana ni vijana wawili raia wa Ujerumani.

Upande wa Hamas nao umesema kundi jingine la wafungwa wa kipalestina walioachiwa na Israel liliwasili salama mjini Ramallah, eneo la Ukingo wa Magharibi. Hayo yamejiri wakati inaarifiwa pande hizo mbili zimeafikiana kurefusha muda wa kusitisha mapigano kwa siku mbili zaidi.

Taarifa hizo zimetolewa na maafisa wa Qatar, taifa linalosimamia mashauriano kati ya kundi la Hamas na Israel. Makubaliano hayo mapya yanasubiri idhini ya serikali ya Israel ili yaanze kufanya kazi kuanzia leo.