Mataifa zaidi yasitisha ufadhili kwa shirika la UNRWA
27 Januari 2024Finland, Italia, Canada na Australia ni mataifa ya hivi karibuni kabisa kuzangaza kusitisha msaada wote wa kifedha kwa UNRWA.
Inafuatia hatua iliyochukuliwa na Marekani mnamo siku ya Ijumaa ambayo nayo ilitangaza kusitisha ufadhili wote kwa UNRWA. Uingereza kwa upande wake imesema inasitisha sehemu ya ufadhili wake kwenye shirika hilo.
Tuhuma zinazolikabili shirika hilo ni kwamba wafanyakazi wake 12 "huenda walishiriki" kutekeleza shambulizi la kundi la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7 mwaka jana. Shambulizi hilo ndiyo ilikuwa chanzo cha kuzuka vita huko Ukanda wa Gaza.
Marekani ilijibu tuhuma hizo siku ya Ijumaa kwa kutangaza mara moja kusitisha ufadhili wote wa kifedha kwa UNRWA.
UNRWA ilisema siku ya Ijumaa kuwa imewafukuza kazi wafanyakazi wake kadhaa walituhumiwa na Israel kushiriki shambulizi la Oktoba 7.
Mkuu wa shirika hilo, Philippe Lazzarini, ameahidi kuwachukulia hatua "ikiwa ni pamoja na kuwashtaki kwa jinai" mfanyakazi yeyote atakabainika kujihusisha na "matendo ya kigaidi".
Uamuzi huo utakuwa pigo kwa juhudi za msaada zinazotolewa kwa Palestina hasa wakati huu wa vita kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas.
Canada na Australia zahimiza uchunguzi mpana
Waziri wa mambo ya kigeni wa Australi Penny Wong amesema siku ya Jumamosi kuwa "amestushwa mno" na madai yaliyotolewa dhidi ya UNRWA.
"Tunazungumza na washiirka na kwa muda tutasitisha fedha tulizopanga kuzitoa hivi karibuni," ameandika Wong kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Mwanadiplomasia huyo wa Australia pia amesema wanazikaribisha hatua zilizochukuliwa na UNRWA "ikiwemo uamuzi wa kusitisha mikataba, na tangazo lake la kuanzisha uchunguzi kamili wa madai hayo dhidi ya shirika hilo".
Kwa upande wake Canada kupitia waziri wa maendeleo ya kimataifa Ahmed Hussen imesema serikali mjini Ottawa "imesitisha kwa muda msaada ziada kwa UNRWA kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazotolewa".
Amesema Canada inazichukulia tuhuma hizo kwa uzito mkubwa na kwamba inashirikiana kwa karibu na UNRWA na wafadhili wengine kutafuta mzizi wa jambo hilo. Canada pia imelitolea mwito shirika hilo la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua nzito haraka iwezekanavyo iwapo itathibitika miongoni mwa wafanyakazi wake walishiriki hujuma dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7.
Palestina yalia na kusitishwa ufadhili kwa UNRWA
Kufuatia uamuzi wa mataifa kusitisha ufadhili wake, serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetoa rai kwa jumuiya ya kimataifa kutowatupa mkono watu wa Palestina na kwamba UNRWA inahitaji "msaada mkubwa".
Waziri wa Ustawi wa Jamii wa Palestina , Hussein Al-Sheikh, ameandika kupitia ukurasa wa mtandao wa X kuwa Palestina inahitaji msaada badala ya kuondolewa misaada.
Israel kwa upande wake imeapa kwamba shirika hilo la Umoja wa Mataifa halitoendelea na kazi yake Ukanda wa Gaza baada ya vita kumalizika. Imesema itafanya kila liwezekenalo kusitisha shughuli zake.
"UNRWA haitokuwa sehemu (ya Gaza) baada ya vita" ameandika waziri wake mambo ya kigeni wa Israel Katz.
Mahusiano kati ya pande hizo mbili yamezorota katika siku za karibuni baada ya UNRWA kusema kombora lililofyetuliwa na kifaru limeipiga moja ya kambi za watu waliopoteza makaazi huku kwenye mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis.
Kundi la Hamas lenyewe limeishambulia Israel kwa kile vimekiita "vitisho" vya nchi hiyo dhidi ya shirika la UNRWA. Kundi hilo linalotawala Ukanda wa Gaza limeitaka Jumuiya ya Kimataifa "kutohadaika na vitisho na ulaghai" wa Israel.