Mataifa yamkosoa Assad na hotuba yake
7 Januari 2013Katika hotuba hiyo Rais al-Assad amefuta uwezekano wa kuwa na mazungumzo na makundi ya upinzani ambayo ameyaita kuwa ni "vibaraka" wa mataifa ya magharibi na ameapa kuendelea kupambana na "magaidi" na "magenge ya wahuni " wanaotaka kuangusha utawala wake.
Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza kwa umma baada ya kipindi cha zaidi ya miezi saba, Rais Assad amewaita wapinzani wake kuwa ni maadui wa wananchi na maadui wa Mungu ambao wameamua kufanya ugaidi.
Tunapambana na magaidi: Assad
Assad ameongeza kusema kwamba wapinzani wanaziita harakati zao kuwa ni mapinduzi lakini kumbe wanachokifanya hakihusiani kabisa na mapinduzi.
"Haya sio mageuzi kwasababu mageuzi kwa kawaida ni harakati za watu na sio vita vya wageni dhidi ya watu. Mapinduzi ni kusimama kwa ajili ya watu na sio dhidi ya watu. Hawa si wanamapinduzi, hawa ni baadhi tu ya wahalifu wa kawaida", alisema Assad.
Wafuasi wake waliokuwa kwenye ukumbi wa jengo la michezo ya kuigiza mjini Damascus walimkatiza mara kwa mara kwa kumshangilia kwa mayowe huku wakisema "Kwa roho na damu yetu tutakulinda Assad."
Katika hotuba hiyo Rais Assad alitaja mpango wa kumaliza vita vinavyoendelea nchini mwake ambao unajumuisha kufanyika kwa mjadala wa kitaifa wa mazungumzo ya amani, chaguzi za bunge na kuandikwa katiba mpya.
Pingamizi dhidi ya Asad
Mara baada ya hotuba ya kiongozi huyo, makundi ya upinzani nchini Syria yalipaza sauti na kukataa mapendekezo yake na kusisitiza kwamba ufumbuzi wa kisiasa kwa mzozo huo hauwezi kufikiwa bila ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo. Rami Abdel Rahman mkuu wa Shirika la Kuangalia Hali za Haki za Binaadamu nchini Syria amesema hakuna nafasi ya kufikia suluhisho wakati serikali hiyo ikiwa madarakani.
Mbali na pingamizi kutoka kwa wapinzani, taasisi za kimataifa na mataifa mbalimbali nayo yamempinga Assad ukiwemo Umoja wa Ulaya. Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja huo Catherine Ashton amesema kuwa Rais Assad ni lazima aachie madaraka ili kurejesha hali ya utulivu na amani nchini Syria.
Ashton amesema kuwa wataichambua kwa makini hotuba ya Assad kuona kama kuna kitu kipya lakini msimamo wao unabaki palepale kwamba inabidi ang´atuke na kuruhusu mchakato wa kuanzisha kipindi cha kisiasa cha mpit
Kama ilivyo kwa Ashton, naye Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alikuwa na haya ya kusema
Naye Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa wito kwa Rais Assad kuviamuru vikosi vyake vya usalama kusitisha mauwaji badala ya kuendelea kutoa hotuba hewa juu ya utayari wake wa kusitisha mapigano. Westerwelle amziita kauli za Assad katika hotuba yake kuwa ni "tupu".
Westerwelle anasema kuwa mwezi Novemba mwaka jana Rais Assad alikiambia kituo cha televisheni cha Urusi kuwa hataondoka nchini humo kwenda uhamishoni kama ilivyosemekana na kwamba ataishi na kufa ndani ya Syria.
"Ujumbe wangu kwa Assad ni “ondoka”. Ana damu nyingi za watu mikononi mwake. Sasa tunajua kuwa watu 60,000 wameuawa Syria. Nimekutana na badhi ya wakimbizi kambini kwenye mpaka wa Jordan. Mambo waliyonieleza yalinishtua sana kuhusu jinsi gain walivyopigwa kwa mabomu na risasi na wakati mwingine hata kutolewa nje ya nyumba zao, vijiji vyao na miji yao"
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba hotuba ya Rais Assad "imepindukia unafiki " na ahadi zake tupu hazitamghilibu mtu yeyote.
Hotuba hiyo imekosolewa pia na Marekani, na Uturuki ambapo zimetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kumtoa Assad madarakani. Licha ya hayo yote, hii leo vikosi vya serikali ya Assad vimefanya mashambulizi mapya katika vitongoji mbalimbali vya mji mkuu Damascus.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Stumai George/Dpa/Afp
Mhariri: Yusuf Saumu