Mataifa yakubaliana kusitisha uhasama Syria
12 Februari 2016Baada ya mkutano mrefu mjini Munich uliyolenga kufufua mazungumzo ya amani yaliyokwama wiki iliyiopita, mataifa hayo yakiwemo Marekani, Urusi na mengine 15 yalisisitiza siku ya Ijumaa, dhamira yao ya kuwepo na kipindi cha mpito wa kisiasa nchini Syria baada ya hali kutengama.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, alikiri kuwa mkutano huo ulitoa ahadi za kwenye makaratasi tu, na kwamba "tunachotaka kukiona katika siku chache zijazo ni utekelezwaji wa maazimio hayo kivitendo," alisema na kuongeza kuwa "bila mpito wa kisiasa, haiwezekani kupata amani."
Kerry alisema pande zote zimedhamiria kwa usitishaji wa uhasama kuanza kutekelezwa ndani ya muda wa wiki moja, na kuongeza kuwa hilo linazihusu pande zote isipokuwa makundi ya Dola la Kiislamu na Jabhat al-Nusra. Alisema wanadiplomasia hao walikubaliana pia kuharakisha na kutanua uwasilishaji wa msaada wa kiutu mara moja katika maeneo yaliyozingirwa.
Urusi kuendeleza mashambulizi
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa Urusi haitasitisha mashambulizi yake ya angani nchini Syria, akihoji kuwa usitishaji mashambulizi hauyahusu makundi kama Dola la Kiislamu na Jabhatu Nusra, linalofungamana na mtandao wa Al-Qaeda.
"Vikosi vyetu vya angani vitaendelea kufanyakazi dhidi ya makundi hayo," alisema Lavrov na kuongeza kuwa "kwa mara ya kwanza katika kazi yetu, nyaraka tulizoziidhinisha leo zinazungumzia umuhimu wa kushirikiana siyo tu katika masuala ya kisiasa na kiutu, lakini pia kijeshi."
Marekani na washirika wake wa Ulaya wanasema ni mashambulizi machache tu ya Urusi yanayoyalenga makundi hayo, na kwamba idadi kubwa ya mashambulizi yanalenga maeneo ya waasi wanaoungwa mkono na mataifa ya magharibi yanayopambana kuuangusha utawala wa rais Bashar al-Assad.
Lavrov alisema mazungumzo ya amani yanapaswa kuanza tena mjini Geneva haraka iwezekanavyo na makundi yote ya upinzani ya Syria laazima yashiriki bila masharti yoyote.
Lakini waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammond, alisema itawezekana kukomesha mashambulizi pale tu Urusi itakapositisha mashambulizi yake kuvisaidia vikosi vya Assad vinavyosonga mbele dhidi ya wapinzani.
Wanadiplomasia wametahadharisha kwamba Urusi hadi sasa haijaonyesha nia yoyote ya kumuona Assad akiondolewa, na kwamba inashinikiza ushindi wa kijeshi.
Hofu ya vita kuu vya dunia
Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev, siku ya Alhamisi alizungumzia uwezekano wa mgogoro usiyosuluhishika au hata vita kuu vya dunia, ikiwa mataifa yatashindwa kujadiliana ukomeshaji wa mapigano nchini Syria, ambayo yameuawa zaidi ya watu 250,000, kusabisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi, na kuliimarisha kundi la Dola la Kiislamu.
Kundi kuu la upinzani la Syria limekaribisha mpango wa mataifa hayo makubwa, lakini limetahadharisha kuwa makubaliano hayo laazima yaonyeshe ufanisi kabla halijajiunga na mazungumzo ya kisiasa na wawakilishi wa serikali mjini Geneva.
Uingiliaji wa Urusi katika uwanja wa vita kwa niaba ya Assad tangu Oktoba iliyopita, umebadilisha mwelekeo wa vita hivyo. Mapambano katika wiki mbili zilizopita yameshuhudia vikosi vya serikali na washirika wao vikiwafurusha waasi na kukaribia kuizingira Aleppo, mji uliyogawanyika ambao nusu yake inadhibitiwa na waasi.
Mazungumzo ya kwanza ya amani katika kipindi cha miaka miwili kati ya pande hasimu yalivunjika wiki iliyopita kabla hata ya kuanza, kutoaka na mashambulizi ya vikosi vya serikali pamoja na Urusi.
Urusi katika mtego wake yenyewe
Mwanadiplomasia wa juu wa Ufaransa alisema: "Warusi walisema wataendelea kuwashambulia magaidi. Wanachukuwa hatari ya kisiasa kwa sababu wanakubalia majadiliano ambao wanaafiki kusitishwa uhasama. Ikiwa ndani ya wiki hakutakuwa na mabadiliko kutokana na mashambulizi yao, basi watabeba dhamana."
Washington inaongoza kampeni yake yenyewe dhidi ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu mashariki mwa Syria na Kaskazini mwa Iraq, lakini imekataa miito ya kuingilia kati katika viwanja vikuu vya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, ambako serikali inapambana kwa sehemu kubwa dhidi ya makundi mengine ya waasi.
Taarifa ya mpango huo uliyofikiwa mjini Munich ilisema mataifa yameunda kikosikazi cha kuratibu usitishaji mapigano, chini ya wa Umoja wa Mataifa, kikiongozwa kwa pamoja kati ya Marekani na Urusi, na kuhusisha wajumbe kutoka upande wa serikali na upinzani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Josephat Charo