1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Sahel kuunda kikosi cha kupambana na wanajihadi

22 Januari 2025

Viongozi wa kijeshi wa nchi tatu za ukanda wa Sahel barani Afrika wametangaza mpango wa kuunda kikosi cha pamoja chenye wanajeshi 5,000 kupambana na vurugu za wapiganaji wa jihadi zilizodumu kwa miaka kadhaa sasa.

https://p.dw.com/p/4pSlZ
Mali, Niger und Burkina Faso gründen eigene Allianz
Picha: Mahamadou Hamidou/REUTERS

Waziri wa Ulinzi wa Niger, Salifou Mody, ametangaza kuundwa kwa kikosi cha pamoja chenye wanajeshi wapatao 5,000 kutoka Niger, Burkina Faso, na Mali, ambacho kinatarajiwa kuanza kazi “ndani ya wiki chache zijazo.”

Kikosi hicho kiko chini ya mwavuli wa muungano mpya unaojulikana kama Alliance of Sahel States (AES), uliobuniwa na nchi hizo tatu ambazo zote zipo chini ya uongozi wa kijeshi kufuatia mapinduzi yaliyotokea kati ya mwaka 2020 na 2023.

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Mody alisema lengo ni kukabiliana na ongezeko la mashambulizi ya vikundi vya wapiganaji vinavyojinasibisha na makundi ya Al-Qaeda na Dola la Kiislamu.

“Kwenye eneo hili la pamoja, majeshi yetu yataweza kufanya operesheni kwa pamoja,” alieleza, akiongeza kuwa kikosi hiki “kimekaribia kukamilika” na kitakuwa na zana za anga, vifaa vya ardhini, pamoja na rasilimali za kijasusi na mifumo ya uratibu.

Tayari operesheni za awali za pamoja zinadaiwa kufanyika katika maeneo yanayopakana, ambako mashambulizi yameripotiwa kuwa mengi zaidi.

Burkina Faso, Ouagadougou | Mkutano wa Mawaziri wa Muungano wa Nchi za Sahel (AES)
Mkutano wa Mawaziri wa Muungano wa Nchi za Sahel (AES), mjini Ouagadougou, Burkina Faso.Picha: Fanny Noaro-Kabré/AFP/Getty Images

Eneo linalojumuisha nchi hizi tatu linakadiriwa kuwa na ukubwa wa takriban kilomita za mraba milioni 2.8—karibu mara nne ya ukubwa wa Ufaransa—na limekabiliwa na changamoto za kiusalama kwa takriban muongo mmoja.

Kujitoa kwa Ufaransa

Tangu mapinduzi yaliyotokea katika nchi hizo, uhusiano na Ufaransa umedorora, hali iliyosababisha kufukuzwa kwa majeshi ya Ufaransa ambayo awali yalikuwa yakisaidia kupambana na vikundi vya wapiganaji.

Soma pia:Togo yasema inaweza ikajiunga kwenye makubaliano ya kiusalama ya Sahel, AES 

Badala yake, Burkina Faso, Mali, na Niger zimejiondoa pia katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na kuamua kujitegemea zaidi, huku zikionyesha nia ya kushirikiana na washirika wapya kama Urusi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), takriban watu milioni 2.6 walikuwa wameyahama makazi yao katika eneo la Sahel kufikia mwisho wa Desemba mwaka uliopita, kutokana na machafuko na ukosefu wa usalama.

Viongozi wa kijeshi wa nchi hizi tatu wanasema kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha AES kutasaidia kuleta ufanisi na ushirikiano imara katika kulinda raia na mipaka yao.

Niger Niamey | Wafuasi wa Muungano wa AES wakisherehekea kujitoa ECOWAS
Wafuasi wa Muungano wa Nchi za Sahel (AES) wakiwa wameinua bango lao wakati wakisherehekea hatua ya Mali, Burkina Faso na Niger kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) huko Niamey, Januari 28, 2024.Picha: Hama Boureima/AFP/Getty Images

“Tuko katika sehemu moja, tunakabiliana na aina moja ya tishio, hususan tishio la makundi ya kihalifu. Tunapaswa kuunganisha nguvu,” Mody alisisitiza.

Soma pia: Je, Ujerumani inapaswa kupanua ushirikiano kanda ya Sahel?

Hatua hii inatazamiwa kuleta matumaini mapya miongoni mwa jamii zinazoathiriwa na mashambulizi ya mara kwa mara, huku Umoja wa Mataifa ukiendelea kutoa wito wa msaada wa kibinadamu.

“Nchi hizi tatu zimeamua kuja pamoja ili kulinda raia wetu na ardhi yetu,” aliongeza Mody, akifafanua kuwa kuanza rasmi kwa kikosi hicho ni suala la muda mfupi ujao.

Viongozi hao wanatarajia mpango huu mpya utafungua ukurasa mpya wa amani na usalama wa kudumu katika ukanda huo wa Sahel.