Norway yahimiza baraza la haki la UN kuchunguza ghasia Sudan
30 Septemba 2023Rasimu ya pendekezo hilo iliyoonekana na shirika la habari la Reuters, inalaani visa vya ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji uliofanywa wakati wa vita vya miezi mitano nchini Sudan.
Rasimu hiyo inanuia kuunda jopo la watu watatu ili kuchunguza ghasia hizo. Jopo hilo limetwikwa jukumu la kuainisha visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kuandika ripoti kwa baraza la Baraza la haki la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 47.
Umwagaji damu, ghasia na visa vya watu kuhama makwao vimeongezeka tangu kuanza kwa vita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha msaada wa dharura RSF mwezi Aprili, na kuipeleka Sudan kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Sehemu zilizoathirika zaidi na vita hivyo ni Darfur Magharibi, ambapo mashambulizi yaliyochochewa kikabila yamesababisha vifo vya mamia ya watu.