1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mataifa ya kiarabu yalaani shambulizi katika ukanda wa Gaza

21 Oktoba 2023

Viongozi wa mataifa ya kiarabu katika mkutano wa kimataifa ulioitishwa na Misri kujadili njia za kumaliza vita kati ya Israel na kundi la Hamas, wamelaani mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza

https://p.dw.com/p/4Xr64
Mkutano wa kimataifa wa amani ya Mashariki ya Kati mjini Cairo, Oktoba 21, 2023
Mkutano wa kimataifa wa amani ya Mashariki ya KatiPicha: The Egyptian Presidency/REUTERS

Kutokuwepo kwa maafisa wakuu wa Israel na Marekani katika mkutano huo, kumedhoofisha matarajio yoyote ya kusitisha vita hivyo vinavyozidi kuongezeka.

Soma pia: Israel yaanza kuwakusanya wanajeshi na polisi wa ziada

Viongozi hao na mawaziri wa mambo ya nje wamekutana wakati ambapo mzozo huo ambao sasa umedumu kwa muda wa wiki mbili unazidi makali na kuzidisha mashaka ya kuzuka janga kubwa la kibinadamu ndani ya Ukanda wa Gaza ambao ni makazi ya takriban watu milioni 2.3.

Mataifa ya Kiarabu yataka kuanza kwa mazungumzo ya kumaliza mvutano kati ya Israel na Palestina

Mataifa hayo ya kiarabu yamesema kuwa sasa ni wakati wa kuanzisha juhudi za kumaliza mvutano wa miongo mingi kati ya Israel na Palestina ambao uligeuka kuwa vita mnamo Oktoba 7 wakati kundi la Hamas lililoorodheshwa na mataifa kadhaa ya magharibi kuwa la kigaidi lilipofanya mashambulizi katika ardhi ya Israel na kusababisha mashambulizi ya kisasi kutoka kwa taifa hilo.