Mataifa ya G7 kutoa msaada zaidi kwa Ukraine
3 Novemba 2022Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amefanya hii leo mazungumzo na mwenzake wa Marekani Antony Blinken katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Münster, saa chache kabla ya kuanza mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizoimarika zaidi kiviwanda G7
Hakuna maelezo ya mazungumzo yao yaliyopatikana mara moja, ingawa kuna uwezekano mawaziri hao wawili walijadili masuala mbalimbali yaliyopo kwenye ajenda ya mkutano wa G7, ikiwa ni pamoja na matukio katika vita vya Ukraine.
Siku hii ya kwanza ya mkutano huo wa siku mbili inatarajiwa kugubikwa na suala la misaada kwa Ukraine, kutokana na mashambulizi ya Urusi ya hivi karibuni dhidi ya miundombinu ya nishati ya nchi hiyo.
Nchi zilizopo katika Kundi hilo la G7 la mataifa yaliyoimarika zaidi kiviwanda ni pamoja na Marekani, Ujerumani, Uingereza, Kanada, Ufaransa, Italia na Japan.
Soma zaidi: Mataifa ya G7 kujadili msaada zaidi kwa Ukraine
Kufuatia mazungumzo hayo baina ya nchi hizo mbili, Baerbock na Blinken walipanga jinsi ya kushiriki katika mjadala kuhusu mustakabali wa demokrasia katika ulimwengu wa kidijitali. Mada ni pamoja na jinsi ya kuidhibiti Urusi kutokana na matumizi yake ya makusudi ya habari potofu na za uwongo.
Majadiliano hayo yanazingatia kongamano la Ujerumani na Marekani, lililozinduliwa mwezi Julai mwaka jana na Rais wa Marekani Joe Biden na Kansela wa Ujerumani wa wakati huo, Angela Merkel.
Kujadiliwa pia: Korea Kaskazini, Urusi, China na Iran
Ujerumani ambayo mwaka huu inashikilia urais wa zamu wa G7, imelaani kwa maneno makali majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini huku ikisema kuwa kundi la G7 halitairuhusu Urusi 'kuwaua njaa' raia wa Ukraine na kusema umoja huo utaratibu msaada kwa Ukraine wakati wa majira ya baridi.
Kabla ya kuanza mkutano huo wa G7, Baerbock amesema hawataruhusu ukatili wa vita hivi kusababisha umati wa wazee, watoto, vijana na familia kufa katika miezi ijayo ya baridi.
Mada inayohusiana:
Aidha Waziri huyo wa Ujerumani amesema kundi la G7 liko tayari kuitambua China kama "mshindani" na "mpinzani" katika kipindi ambacho Japan inajiandaa kuchukua urais wa zamu wa kundi hilo.
Aidha, Baerbock amesema Japan imekuwa ikisisitiza mara kwa mara jinsi ilivyo muhimu kutambua kuwa China imebadilika katika miaka ya hivi karibuni na kwamba sio tu mshirika katika masuala ya kimataifa lakini pia mshindani na mpinzani.
Katika mkutano huo wa siku mbili unaoanza leo Alhamisi, viongozi hao wa G7 watajadili pia kuhusu ukandamizaji wa Iran dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu, pamoja pia na ukuaji wa uchumi wa taifa la China na malengo yake juu ya kisiwa cha Taiwan.
Hayo yanajiri wakati Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anafanya ziara mjini Beijing wiki hii, na kuwa kiongozi wa kwanza wa bara la Ulaya kuitembelea nchi hiyo tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine.