IOM: Mataifa tajiri yanawahitaji sana wahamiaji
2 Oktoba 2023Amy Pope ameanza uongozi wake wa shirika la IOM akijenga hoja ya jinsi uhamiaji ulivyo na manufaa kwa mataifa tajiri ambayo raia wao wanazidi kuzeeka na nguvukazi yao inazidi kuporomoka.
Pope aliwaambia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva siku ya Jumatatu (Oktoba 2), kwamba wanasiasa wanaopingana na uhamiaji katika mataifa ya Magharibi hawazingatii uhalisia uliomo kwenye chumi za mataifa yao "ambazo zinanufaika pakubwa na wahamiaji."
"Ushahidi uliopo ni kwamba uhamiaji unayafaidisha kiuchumi mataifa yanayohamiwa. Ukiangalia mataifa ambayo yamekuwa na wimbi kubwa la wahamiaji kwa miaka mingi, ukiangalia namna chumi zake zinavyofanya vyema, tunaweza kuona zinaimarika kwa sababu ya uhamiaji. Ama kwa kuchochea ubunifu, au idadi ya nguvukazi, ama ugunduzi au kujaza ombwe la jamii inayozeeka, uhamiaji kwa ujumla wake una faida." Alisema Pope.
Soma zaidi: Viongozi wa nchi tisa za Mediterania wahimiza Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kuzuia uhamiaji kwenye chanzo
Idadi ya watu wanaokimbia makwao kukimbilia mataifa mengine kusaka maisha mazuri imekuwa ikiongezeka kila uchao, huku baadhi ya serikali zikijaribu kutekeleza sera ya kuwapokea, lakini zikikabiliwa na upinzani mkali wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia.
Serikali ya Marekani, ambayo ilimuunga mkono Pope kwenye kuwania uongozi wa IOM, imetowa hivi karibuni vibali vya kazi kwa raia 500,000 wa Venezuela, ambao nchi yao imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni.
Upinzani dhidi ya wahamiaji
Lakini wakosoaji wanasema sera kama hizo zinashajiisha wahamiaji kujazana nchini Marekani, ambako wanafanya kazi za vibarua na za malipo duni na hivyo kushusha thamani ya kazi na mishahara mizuri kwa wenyeji.
Hata hivyo, Pope alisisitiza kwamba mataifa yanapaswa kuhakikisha yanatayarisha njia halali kwa wahamiaji kuingia, kama ulivyo msimamo wa muda mrefu wa taasisi za Umoja wa Mataifa.
Soma zaidi: UN: Wahamiaji waliokufa au kupotea baharini yaongezeka 2023
Alisema shirika lake lina wasiwasi mkubwa na vifo vya wahamiaji kama inavyotokea kwenye Bahari ya Mediterenia, ambavyo sasa vimefanywa jambo la kawaida kama kwamba wanaokufa si binaadamu kamili.
"Tunachotaka ni kubadilisha huu mtazamo, tujuwe kuwa hawa ni wanaadamu kwanza kabla hatujawapa majina ya wahamiaji haramu, au waomba hifadhi, au jengine lolote. Kuufahamu ubinaadamu, uhai na utu wao, ndiko kuwe msingi wa kila tunakichosema na kuwafanyia."
Pope, aliyeanza majukumu yake kama mwanamke wa kwanza kuongoza IOM siku ya Jumapili (Oktoba 1), alichukuwa nafasi iliyokuwa inashikiliwa na mkuu wake wa zamani, Antonio Vitorino, kutoka Ureno.
Tangu mwaka 1951 lilipoundwa shirika hilo, ambalo sasa lina mataifa wanachama 175 na wafanyakazi zaidi ya 20,000, limewahi kuwa na wakuu wawili tu ambao si raia wa Marekani.
Vyanzo: AP, Reuters