Maswali na majibu bungeni mara ya kwanza Ujerumani
7 Juni 2018Mara nyingine wabunge walinapaswa kufanya utafiti kwanza kabla ya kuuliza maswali. Hata hivyo inaonekana kwamba wabunge kama inavyofahamika walikuwa wanajipasha moto tu. Hakukuwa na mjadala mkali katika kikao hiki cha maswali na majibu. Ndio sababu kansela aliweza hata kuwaaga wabunge kwa kuwafinyia jicho na kusema , "nitakuja tena". Huenda hiyo ni ishara ya kuwatuliza.
Gazeti la Rhein-Zeitung la mjini Koblenz likiandika kuhusiana na tukio hilo la maswali na majibu bungeni , linasema wabunge wamepoteza fursa, kumhoji kwa kina kansela. Mhariri anaandika:
Ili kikao hicho cha maswali na majibu kivutie zaidi, na kuweza kufahamisha zaidi , wauliza maswali walipaswa kuwa na ufahamu mkubwa zaidi na kuuliza maswali magumu. Ilipaswa iwe ni mjadala, mazungumzo yenye mapambano, na mivutano. Makundi ya wabunge yalipaswa kuwa werevu zaidi, na kulenga katika mada moja zaidi na kuuliza maswali zaidi ya kuchokonoa na magumu. Maswali aliyotupiwa kansela pamoja na mawaziri yalikuwa kama kumsalimia tu. Mfumo huo kwa kweli haujakuwa wa mafanikio. Wabunge wanahitaji uhuru zaidi, ili kuweza kuuliza maswali mazito na kupambana na majibu ya juu juu ya yanayotolewa na kansela.
Mambo mawili muhimu hayapaswi kupuuziwa: anaandika mhariri wa gazeti la Mannheimer Morgen , kuhusiana na uchaguzi wa rais na bunge nchini Uturuki. Mhariri anaadika:
Kwanza ni kwamba rais Erdogan na chama chake cha AKP amefanikiwa hapo nyuma kupitia mageuzi kuibadilisha Uturuki kiuchumi na kuleta hali bora kwa wananchi wake. La pili ni kwamba mbali na kuleta hali ya kuwa ni kiongozi anayeelekea kuwa mtawala anayejilimbikizia madaraka lakini ni mmoja kati ya wale walioleta uthabiti nchini mwake. Upinzani umegawanyika, Waturuki katika miongo iliyopita walishuhudia mapinduzi kadhaa na kuvunjika kwa serikali. kutokana na hayo kunatokea hali ya wasi wasi katika mataifa jirani kama vile Syria ama hata Iraq.
Mada ya mwisho inahusu Mjerumani Alexander Gerst aliyesafiri kwenda katika kituo cha anga cha kimataifa angani ISS. Gazeti la Mittelbayerische Zeitung la mjini Regensburg linaandika:
Gerst ni mtu anayeleta furaha kwa shirika la Ulaya la mambo ya anga ESA pamoja na shughuli za safari za anga za juu kwa jumla. Kuna watu kama yeye ama mwanaanga wa canada anayependelea kupiga gitaa Chris Hadfield , ambao wamefanikiwa , kuamsha hamasa kubwa kwa watu wengi , kuhusu mambo ya anga za juu na utafiti katika kituo cha ISS. Ndio sababu ni muhimu , kwa kuwa mpango wa safari za anga za juu ni ghali , na baadhi hujiuliza iwapo fedha hizo zisingetumika vizuri hapa ardhini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse /
Mhariri: Iddi Ssessanga