Masoko ya hisa yahofia wimbi la pili la maambukizi ya Corona
11 Juni 2020Wafanyabiashara pia wameguswa na hofu ya wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya corona nchini Marekani na kwingineko duniani. Hii ni kutokana na ongezeko jipya la maambukizi katika baadhi ya majimbo.
Masoko ya hisa yamekuwa yakifanya vizuri kwa wiki kadhaa wakati hatua za kuwazuwia watu kutoka majumbani mwao zikilegezwa hatua kwa hatua katika maeneo muhimu, na baada ya serikali na benki kuu za nchi kuahidi matrilioni ya dola kusaidia kuzindua ukuaji wa uchumi wao.
Lakini baada ya mkutano uliokuwa ukitupiwa jicho kwa karibu, wizara ya fedha iliweka mtazamo wake kwamba uchumi huo mkubwa duniani utachukua muda kuweza kurejea kikamilifu katika hali yake ya kawaida kutokana na dharura hii ya janga la virusi vya corona ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa vizazi kadhaa, hali ambayo inatarajiwa kuielekeza dunia katika mdororo wa uchumi.
Jumla ya idadi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Marekani imepindukia milioni 2 hadi jana, kwa mujibu wa idadi iliyowekwa pamoja na shirika la habari la Reuters, huku shughuli za kawaida zikirejea hatua kwa hatua katika majimbo mengi.
Maambukizi zaidi Urusi
Maambukizi ya virusi vya corona nchini Urusi imepindukia watu laki tano leo baada ya maafisa wa afya kuripoti maambukizi mapya yanayofikia watu 8,779. Urusi ina jumla ya wtu 502,436 waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19, ikiwa ni pamoja na vifo 6,532.
Licha ya kurekodi karibu maambukizi mapya 9,000 kwa siku kwa zaidi ya mwezi mmoja, maafisa nchini Urusi wameanza kulegeza vizuwizi vya watu kusalia majumbani katika majimbo mengi, ikiwa ni pamoja na Moscow, ambayo ina asilimia 40 ya wagonjwa wote kwa jumla na karibu nusu ya vifo vilivyoripotiwa.
Serikali ya mji wa Tokyo inapanga kuruhusu biashara kufunguliwa tena kuanzia Juni 19, wakiondoa maombi ya kuendelea kuwazuwia watu kutoka majumbani mwao iliyotoa ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.
Tanzania yatakiwa kutoa data
India imeripoti kiwango cha juu cha maambukizi cha karibu watu 10,000 wapya walioambukizwa virusi vya corona leo, ambapo huduma za afya katika miji iliyoathirika zaidi ya Mumbai , New Delhi na Chennai ikiendelea kupata maambukizi zaidi.
Mkuu wa kituo cha udhibiti wa magonjwa barani Afrika amesema tunaendelea kuwa na matumaini kuwa Tanzania itatoa ushirikiano kwa kutoa data za mambukizi ya virusi vya corona nchini humo hata iwapo rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli alitangaza ushindi dhidi ya janga hilo.
John Nkengasong amesema wanaelewa maslahi yaliyopo, katika taifa hilo la Afrika mashariki, ambalo halijatoa idadi mpya ya data za virusi vya corona tangu mwishoni mwa mwezi Aprili.