Mashambulizi ya wanamgambo yanaongezeka Pakistan
13 Septemba 2024Pakistan inakabiliwa na ongezeko kubwa la mashambulio ya wanamgambo. Watu 757 waliuawa na wengine idadi kama hiyo walijeruhiwa katika miezi minane ya kwanza ya mwaka huu kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na taasisi ya nchini Pakistan inayoshughulikia migogoro na masuala ya usalama.
Wachambuzi wanasema watu 254 waliuawa mnamo mwezi Agosti pekee, wakiwemo raia 92 na maafisa wa usalama 52. Huo ulikuwa mwezi wa maafa makubwa kabisa katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Wapiganaji hao wanafanya mashambulio hasa kwenye majimbo ya Khyber Pakhtunkhwa na Balochistan, yaliyopo kwenye mpaka na Afghanisan.
Mara kwa mara Pakistan imekuwa ikilishutumu kundi la Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) lenye makao yake nchini Afghanistan, ambalo ni muungano wa makundi yenye itikadi kali, kwa kuendesha operesheni ndani ya Pakistan.
Soma pia:Polisi nchini Pakistan yawashikilia wabunge kadhaa wa Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan
Hata hivyo utawala wa Taliban mjini Kabul umezikanusha shutuma hizo. Kundi jingine la waasi la Baloch Liberation Army (BLA) limeibuka kuwa tishio kubwa miongoni mwa wanamgambo wenye silaha kwenye jimbo la Balochistan.
Kundi hilo la BLA linapigania uhuru wa jimbo hilo lenye utajiri wa raslimali. Pia linapinga miradi inayofadhiliwa na China, ikiwa pamoja na bandari na migodi ya dhahabu na shaba.
Usalama umepungua nchini Pakistan kila mwaka tangu Taliban kutwaa tena mamlaka nchini Afghanistan mnamo 2021.
Lakini mwezi uliopita mashambulio yalizidi mara tatu katika jimbo la Balochistan ambapo wapiganaji wanaotaka kujitenga waliwaua raia zaidi ya 70 katika mashambulizi yaliyopangwa kulenga vituo vya polisi, reli na barabara kuu katika jimbo lote.
Wachunguzi: Mashambulizi yanahatarisha usalama
Mashambulio hayo mabaya mno yalifanyika kwenye maeneo mengi. Wachunguzi wametahadharisha kuwa hujuma hizo zinaweza kuathiri usalama, uchumi na sekta nyingine za jamii kwa kiwango kikubwa.
Hali hiyo imesababishwa na uzembe wa serikali.
Mafanikio yaliyopatikana baada ya kuwatimua wanamgambo hao nje ya nchi hayakudumishwa amesema Ihsanullah Tipu Mehsud, mwanzilishi mwenza wa jukwaa la waandishi habari lisiloegemea upande wowote.
Amesema hakuna utaratibu uliowekwa kwa kushirikiana na Afghanistan wakati wa serikali ya Ashraf Ghani, na hivyo hali hiyo imetoa nafasi kwa TTP ya kujipanga na kujenga nguvu tena.
Mwanadiplomasia wa zamani wa Pakistan na mchambuzi wa sera za nje Maleeha Lodhi, anaamini kuwa utawala wa Taliban umeshindwa kuchukua hatua dhidi ya wapiganaji hao.
Soma pia:Jeshi la Pakistan laanzisha operesheni dhidi ya waasi wa Balochistan
Pana sababu kadhaa za kuongozeka kwa mashambulio ya wapiganaji ndani ya Pakistan. Na sababu kubwa ni msimamo wa Taliban kukataa kuwadhibiti wanamgambo hao wanaoendelea kufanya hujuma kutokea Afghanistan.
Mnamo mwezi wa Julai, Umoja wa Mataifa uliiorodhesha, TTP kuwa kundi la kigaidi nchini Afghanistan linalofadhiliwa kwa kiwango kikubwa na watawala wa nchi hiyo ili kuweza kufanya mashambulio ndani ya Pakistan.
Mwanazuoni wa taasisi ya Brookings Madiha Afzal, anakubaliana na hoja kwamba watawala wa Afghanistan wanawaunga mkono magaidi hao kwa hali na mali.
Lakini wakati huo huo anawalaumu viongozi wa Pakistan kwa kuendekeza malumbano baina yao na kwa kutumia mkono wa chuma kuwaandama wapinzani wakati uchumi wa nchi unaenda mrama.
Wachambuzi wanaamini kwamba serikali inapaswa kuwa na msimamo thabiti katika kuwakabili wapiganaji hao, pia kwa njia ya kuushirikisha umma wa Pakistan na wadau wengine wote.