1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Mashambulizi ya wanajihadi Mali yazusha ukosoaji, maswali

18 Septemba 2024

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS imelaani vikali mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi yalioukumba mji mkuu wa Mali ambako maswali yamesalia kuhusu shambulio hilo la nadra.

https://p.dw.com/p/4koCX
Mali Bamako | Mkuu wa Majenerali ya Mali Oumar Diarra akizungumza baada ya kushambuliwa kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi
Mkuu wa majeshi ya Mali Oumar Diarra (katikati) akizungumza na vyombo vya habari mjini Bamako.Picha: ORTM/AFP

Operesheni hiyo ya wapiganaji ilikuwa ya kwanza ya aina yake katika miaka kadhaa, ambamo mji mkuu wa Bamako umekuwa ukisazwa na mashambulizi kama hayo yanayotokea karibu kila siku katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Miongoni mwa yasiojulikana bado ni idadi ya watu walioathirika, huku mamlaka zikiwa bado hazijatoa idadi halisi ya vifo.

Uongozi wa jeshi la Mali ulikiri Jumanne usiku kwamba baadhi ya wau walipoteza maisha yao, hasa wanajeshi waliokuwepo kwenye kituo cha mafunzi ya polisi-jeshi.

Ulithibitisha kamba shabaha za mashambulizi hayo zilikuwa kituo hicho cha mafunzo ya askari na uwanja wa ndege wa mji huo.

"Shambulizi hilo lilizuwiwa, washambuliaji kuuliwa na hali kurejeshwa haraka chini ya udhibiti", limesema jeshi la Mali.

Hata hivyo kiwango cha uharibu kufuatia mashambulizi hayo bado hakijajulikana, na maafisa wa serikali na mwandishi wa habari wa shirika la AFP waliripoti kuwa milio ya risasi iliendelea kwa sehemu kubwa ya siku ya Jumanne.

Mali Bamako | Silaha zilizonaswa baada ya kushambuliwa kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi
Baadhi ya silaha zilizokamatwa na jeshi mjini Bamakao, kufuatia shambulizi la wapiganji wa jihadi.Picha: ORTM/AFP

Mshirika wa Al-Qaeda adai kuua mamia ya wanajeshi

Kundi la Jama'at al-Islam wal Muslimeen, JNIM, ambalo lilidai kuhusika na mashambulizi hayo, lilirusha picha  mtandaoni zikionyesha wapiganaji wakirandaranda na kufyatua risasi hovyo kwenye madirisha ya jumba la ndege la rais katika uwanja wa ndege.

Soma pia:Kituo cha mafunzo ya kijeshi Mali chashambuliwa 

Video moja ilimuonyesha mpiganaji akiwasha moto kwenye upande moja wa ndege. Lakini maafisa hawajatoa ishara yoyote iwapo ndege inayomilikiwa na kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita ndiyo iliyolengwa.

Kundi la JNIM limedai kwamba dazeni chache za wapiganaji wake waliua na kujeruhi mamia ya wanajeshi wa serikali, wakiwemo wanachama wa kundi la Urusi la Wagner.

Kundi hilo la jihadi lilisema katika taarifa kupitia chaneli zake za mawasiliano kwamba lili limeharibu ndege sita za kijeshi, ikiwemo droni, na kuharibu nyingine nne. Hata hivyo madai hayo hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Jeshi la Mali ladhibiti usalama baada ya shambulio Bamako

ECOWAS yalaani "vikali mashambulizi" dhidi ya Bamako

Mali inayotawaliwa kijeshi baada ya mapinduzi ya kufuatana ya mwaka 2020 na 2021, imekuwa ikikabiliana na makundi mbalimbali yenye mafungamano na Al-Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu.

Mwandishi wa AFP amesema maduka yameanza kufungua Jumatano katika eneo linalozunguka kambi ya polisi-jeshi, lakini barabara kuu inayopita mbele ya kambi hiyo ilisalia kufungwa ikiwa chini ya uangalizi wa polisi.

Soma pia: ECOWAS yasikitishwa kukosekana muafaka na serikali za kijeshi

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, imelaani vikali mashambulizi dhidi ya Bamako, ambayo utawala wake wa kijeshi unasema unajiondoa kwenye chombo hicho cha kikanda.

Viongozi wa kijeshi wa Mali walivunja uhusiano na jumuiya hiyo mwezi Januari, wakati sawa na mataifa jirani yanayoongozwa kijeshi ya Burkina Faso na Niger.

Mataifa hayo matatu yanaituhumu ECOWA kushindwa kuyaunga mkono katika mapambano yao dhidi ya makundi ya wanajihadi, na kuwa kibaraka wa mkoloni wao wa zamani, Ufaransa.