1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Marekani vyafanya mashambulizi Syria

3 Februari 2022

Vikosi maalumu vya jeshi la Marekani vimefanya kile ambacho makao makuu ya jeshi Pentagon, imekitaja kuwa operesheni kubwa yenye ufanisi ya kupambana na ugaidi, kaskazini-mashariki mwa Syria

https://p.dw.com/p/46TL5
Syrien | Trauer und Zerstörung nach Luftangriff | TABLEAU
Picha: Muhammed Said/AA/picture alliance

Wahudumu wa kwanza kwenye eneo la tukio wameripoti kuwa watu 13 wameuawa, wakiwemo watoto sita na wanawake wanne.

Operesheni hiyo ambayo wakaazi wanasema ilidumu kwa karibu masaa mawili, ilikitikisa kijiji cha Atmeh karibu na mpaka wa Uturuki, kilicho na kambi kadhaa za wakimbizi wa ndani kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.

soma zaidi:Vita vya Syria vilisababisha vifo 3,700 mwaka wa 2021

Shabaha ya uvamizi huo haikubainika wazi mara moja. Msemaji wa Pentagon John Kirby amesema katika taarifa fupi kuwa operesheni hiyo ilikuwa na ufanisi, na kuahidi kutoa taarifa zaidi kadiri zitakapopatikana.

Wakaazi kadhaa hata hivyo, wameripoti kuona vipande vya miili vikiwa vimetapakaa karibu na eneo la tukio, ambalo ni nyumba katika mkoa unaodhibitiwa na waasi wa Idlib.