Mashambulizi ya magaidi wa Msumbiji kusini mwa Tanzania
27 Oktoba 2021Shambulio la kwanza linatajwa kuwa lilifanywa Oktoba 18 katika kijiji cha Sengele, mkoa wa Mtwara. Na la pili lilifanywa Oktoba 21 dhidi ya kijiji cha Kilimahewa, karibu na mto Ruvuma ulio kwenye mpaka wa Msumbiji na Tanzania.
Akizungumza na DW, Abudo Gafuro, kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Kijamii na Kiuchumi Msumbiji (IESE) ya jimboni Cabo Delgado, amesema taarifa hizo zimetolewa na wakimbizi wa Msumbuji waliokuwa wamekimbilia Tanzania na ambao sasa wameanza kurudi mjini Palma.
Soma zaidi: Wanajeshi wa nchi za jumuiya ya SADC kupelekwa Msumbiji
Mashuhuda hao wamethibitisha kutokea kwa mashambulizi katika baadhi ya vijiji vya Tanzania na maeneo mengine yaliyo kaskazini mwa Msumbiji.
"Kwa sasa ni mapema mno kutoa jawabu la uhakika, kwa sababu bado tunafanya kazi na pande zote mbili za Tanzania na Msumbiji kujua ukweli wa taarifa hizo. Hatujui kama kuna waathiriwa, lakini risasi zilifyatuliwa," alisema Abudo Gafuro alipoulizwa na DW kama kuna watu waliouawa kwenye mashambulizi hayo.
Washambuliaji hao wanatajwa kuwa walichoma moto ghala ya korosho na nyumba kadhaa. Halikadhalika kuna taarifa za watu kutekwa nyara, ambao baadae waliokolewa na Kikosi cha Ulinzi cha Tanzania.
Tanzania yakana taarifa hizo za mashambulizi
Inaaminika kwamba makundi hayo ya kigaidi yanakimbia kutoka jimbo la Cabo Delgado kupitia mto Ruvuma, baada ya kuzidiwa nguvu na vikosi vya ulinzi vya Msumbiji vikisaidiwa na washirika wao kutoka Rwanda pamoja na ujumbe maalumu wa Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC wanaopambana kumaliza ugaidi katika eneo hilo.
Ili kupata uthibitisho wa taarifa hizo kwa upande wa Tanzania, DW pia imezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mtawara Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliyesema kuwa hali ni shwari na hadi sasa hakupokea taarifa za aina hiyo.
Soma zaidi:Wanajeshi wa Msumbiji wakomboa raia 87 katika mji wa Pemba
Lakini Gafuro anasisitiza kwamba ushahidi wote unaashiria kutokea kwa mashambulizi hayo wiki iliyopita, kwani anasema magaidi wanatapatapa na hawana pakukimbilia ispokuwa nchi jirani ya Tanzania. "Ni dhahiri wanapokimbilia ni Tanzania, kwa sababu ni moja ya milango wanayotumia kuingilia Msumbiji," aliongeza Gafuro.
Mwanzoni mwa mwezi huu, viongozi wa jumuiya ya SADC, walikubaliana kuongeza muda wa vikosi vyake kuendelea kuwepo Msumbiji kuisadia serikali kupambana na makundi ya siasa kali.
Jumuiya hiyo ya nchi wanachama 16 haijawahi kuweka wazi idadi ya wanajeshi waliopelekwa Msumbiji tangu operesheni yao ilipoanza mwezi Julai.
Machafuko hayo ya wanamgambo yamesababisha vifo vya watu 3,340 na zaidi ya watu 800,000 wamelazimika kuyahama makazi yao.