1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yawaua watu 40 nchini Lebanon

7 Novemba 2024

Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon yamewaua watu 40 kwenye maeneo ya mji wa kusini wa Baalbek huku mashambulizi zaidi yakivilenga viunga vya mji mkuu, Beirut.

https://p.dw.com/p/4mj2C
Mashambulizi ya Israel kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Mashambulizi ya Israel kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut.Picha: FADEL ITANI/AFP

Wizara ya Afya ya Lebanon ndiyo imetoa takwimu za vifo vya watu kwenye hujuma zilizoulenga mji wa Baalbek na kuongeza kwamba watu wengine 53 wamejeruhiwa.

Israel na kundi la Hezbollah la nchini Lebanon wamekuwa wakipambana kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kuzuka kwa vita vya Gaza, lakini makabiliano yameongezeka tangu mwezi Septemba kwa Israel kuzidisha mashambulizi dhidi ya ngome za Hezbollah kusini na mashariki mwa Lebanon.

Hapo jana mbali ya mashambulizi ya mji wa Baalbek, Israel ilipambana pia na Hezbollah kwenye viunga vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, kwa kufanya mashambulizi yasiyopungua manne. Hakuna taarifa za vifo wala majeruhi zilizotolewa kuhusu mashambulizi hayo.

Hujuma hizo zimefanyika saa chache baada ya kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, kusema haamini kwamba suluhisho la kisiasa litamaliza uhasama baina ya pande hizo mbili.