1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Cologne yaratibiwa

10 Januari 2016

Waziri wa Sheria wa Ujerumani Heiko Maas anaamini kwamba mashambulizi dhidi ya wanawake mjini Cologne wakati wa Mkesha wa Mwaka Mpya yaliratibiwa na kupangwa kabla.

https://p.dw.com/p/1Hb1J
Waziri wa Sheria wa Ujerumani Heiko Maas.
Waziri wa Sheria wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/J.Carstensen

Maas amenukuliwa na gazeti mashuhuri nchini Ujerumani la Bild akisema "hakuna anayeweza kuniambia kwamba hayakuratibiwa au kupangwa kabla."Maas pia hakuwa tayari kufuta uwezekano wa kuwepo kwa uhusiano kati ya mashambulizi hayo ya Cologne na yale yaliyotokea katika miji mengine ya Ujerumani usiku huo huo.

Ameliambia gazeti hilo uhusiano wote lazima uchunguzwe kwa makini kutokana na tuhuma ya kuchaguliwa kwa tarehe maalum na idadi ya watu waliokuwa wakitegemewa kujitokeza.

Maas alikuwa anayatilia mkazo matamshi aliyoyatowa mapema wiki hii.Wakati huo huo Maas amewaonya wananchi dhidi ya kuwahusisha kwa jumla wahamiaji wakiwemo raia wenye kutii sheria na mashambulizi hayo baada ya repoti ya polisi kusema kwamba wengi wa watuhumiwa walikuwa wahamiaji wanaotafuta hiafdhi au watu wanaoishi nchini Ujerumani kinyume na sheria.

Malalamiko ya mashambulizi yaongezeka

Malalamiko kuhusiana na mashambulizi hayo yameongezeka maradufu na kufikia 379 kutoka yale yaliyorekodiwa awali ya 170.Takriban wanaume 1,000 inaotajwa kuwa wamelewa inaelezwa kuwa wamewapora kuwanyanyasa kingono na katika matukio mengine kuwabaka wanawake wakati wa shamra shamra za mkesha wa mwaka mpya.

Mkesha wa mwaka mpya Cologne. (21.12.2015)
Mkesha wa mwaka mpya Cologne. (21.12.2015)Picha: Getty Images/AFP/M. Böhm

Wimbi la uhalifu huo wa mwaka mpya mjini Cologne linatajwa pia kutokea katika mji wa Hamburg ambapo kumeripotiwa matukio hayo ya kihuni 108 wakati miji mengine licha ya kutokea visa hivyo havikuwa vingi kiasi hicho.

Amesema ni upuuzi kuvichukulia vitendo hivyo vya uhalifu kama ni ushahidi kwamba wageni hawawezi kujumuishwa katika jamii ya Ujerumani.Pia amesema ni kosa kabisa kuweka uhusiano wowote ule kati ya yale yaliyotokea Cologne na kuwasili kwa wakimbizi milioni moja nchini Ujerumani hapo mwaka 2015.

Amekiri kwamba bila ya shaka ni miongoni mwa zaidi ya watu milioni moja wale ambao walitenda uhalifu lakini hakuna dokezo kwamba visa vya uhalifu vimeongezeka bila ya kiasi tokea kuwasili kwa wimbi hilo la wakimbizi nchini.

Sheria kali kwa wahamiaji

Kansela Angela Merkel akichangia mjadala mkali hapo Jumamosi kuhusu suala hilo amehahidi kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya wahalifu wenye uraia wa kigeni ikiwa ni pamoja na kuwapokoya haki yao ya kuomba hifadhi.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/F. Erichsen

Kiongozi wa kundi la bunge la chama cha SPD Thomas Opperman amesema Jumapili washirika wanaounda serikali ya mseto nchini Ujerumani hawapaswi kutumbukia kwenye mzozo wa itikadi katika suala hilo.

Amesema ana uhakika madai ya chama hicho cha SPD ya kuwepo kwa wafanyakazi na video za uchunguzi yatashughulikiwa kwa haraka.

Siku zijazo chama cha SPD kitashirikiana na washirika wezao katika serikali ya mseto chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel kuwasilisha nsheria mpya katika bunge la Ujerumani Bundestag ambazo zitaweza kuharakisha kurudishwa makwao kwa waomba hifadhi na wahamiaji waliotenda uhalifu.

Serikali imekuwa ikishutumiwa vikali kwa kutojiandaa vyema wakati ilipopitisha sera yake ya kufunguwa milango kwa wahamiaji ili kukabiliana na mzozo wa wahamiaji barani Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mahariri : Grace Kabogo