1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya ADF yasababisha vifo vya watu 12 Kongo

2 Januari 2025

Mashambulizi mapya ya wapiganaji wa kundi la waasi wa ADF linalodai kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi lijiitalo Dola la Kiislamu, IS, yamewaua zaidi ya watu 12 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4okea
DR Kongo | Wanajeshi | Beni
Wanajeshi wa Kongo wakishika doria BeniPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Mashambulizi hayo yanatokea baada ya mkururo wa mashambulizi mengine ya ADF katika kipindi cha Krismasi yaliyowaua watu 21 katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Maafisa wa eneo hilo wamesema mashambulizi hayo yametokea usiku wa kuamkia Jumatano na yalilenga maeneo mawili katika jimbo moja.

Soma pia: Watu 10 wauawa katika shambulio la ADF mashariki mwa Kongo 

Afisa mmoja, Samuel Kagheni, amelieleza shirika la habari la AFP kwamba waasi hao waliwaua watu wanane katika kijiji cha Bilendu.

Watu wengine wanne waliuawa katika kijiji cha Mangoya, huku waasi wakichoma moto nyumba katika maeneo yote mawili.