1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi mapya ya anga yafanyika Aleppo

Isaac Gamba
17 Novemba 2016

Vikosi vya serikali ya Syria kwa ushirikiano wa ndege za kivita za Urusi vimefanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa yanayodhibitiwa na waasi kaskazini mwa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na katika mji wa Aleppo.

https://p.dw.com/p/2SoZC
Syrien Krieg - Luftangriffe in Aleppo
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/J. al Rifai

Mashambulizi hayo mapya yamewaua kiasi ya watu 35 katika mji wa Aleppo katika kipindi cha saa 24 na hivyo kushutumiwa vikali na Marekani na Umoja wa Mataifa huku yakifanyika saa kadhaa baada ya Rais Bashar al-Assad kusema kuwa Rais Mteule wa Marekani Donald Trump anaweza kuwa mshirika wa kweli iwapo atapambana dhidi ya ugaidi.

Syria inawachakulia wale wote wanaoipinga serikali ya Rais Bashar al-Assad kuwa ni magaidi kama vile kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu ambalo Trump amesema utawala wake utajikita zaidi katika kuchukua hatua za kulisambaratisha pale Marekani inapojihusisha na mgogoro wa Syria.

Vikosi vya serikali ya Syria na majeshi washirika ya Urusi walianzisha mashambulizi hapo jana katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi na hivyo kutibua hali iliyokuwepo ya utulivu kwa karibu kipindi cha mwezi mmoja katika mji wa Aleppo mashariki mwa nchi hiyo. Hata hivyo Urusi imekanusha kufanya mashambulizi katika mji huo.

Urusi yakanusha kuhusika na mashabulizi hayo

Syrien Krieg - Luftangriffe in Aleppo
Sehemu ya maeneo yaliyoshabuliwa katika mji wa AleppoPicha: picture-alliance/Anadolu Agency/J. al Rifai

"Ndege za vikosi vya anga vya Urusi hazijafanya mashambulizi katika mji wa Aleppo katika kipindi cha siku 29 zilizopita " alisema Igor Konashenkov, msemaji wa wizara ya ulinzi ya urusi.

Shirika la waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema watoto sita ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi hayo.

Wakati huo huo, Shirika la madakitari huru nchini humo limesema mashambulizi hayo yaliyofanywa kwa kutumia mabomu ya mapipa yameharibu maeneo ya huduma za afya yanayosimamiwa na shirika hilo ikiwa ni pamoja na hospitali ya watoto pamoja na benki pekee ya damu katika eneo hilo.

Vituo vya huduma ya tiba vimekuwa vikilengwa zaidi na mashambulizi ya mara kwa mara na wakati mwingine kuharibiwa kabisa katika operesheni ya vikosi vya serikali ya Syria dhidi ya waasi ingawa serikali ya Syria na Urusi wanakanusha mashambulizi hayo kulenga hospitali.

Shirika hilo la waangalizi wa haki za binadamu limeripoti kuwa kiasi ya watu 21 wameuawa katika kijiji cha Batabo kilichoko mpakani mwa mji wa Aleppo na jimbo la Idlib ambako vikosi vya Syria pamoja na Urusi vimekuwa vikifanya mashambulizi ya anga.

Shirika hilo limesema halikuwa na taarifa za mara moja za uhakika zaidi kama mashambulizi ya anga katika kijiji cha Batabo yalifanywa na ndege za kiita za Urusi au Syria.

Mashambulizi hayo yamemaliza hali ya utulivu iliyokuwepo kwa muda hasa mashariki mwa Aleppo ambako Oktoba 18 mwaka huu Urusi ilisimamisha mashambulizi yake ya anga.

Hatua ya usitishaji mapigano ilikuwa inalenga kuwashawishi wakazi katika maeneo ya mji huo pamoja na waasi kuondoka  ingawa ni wachache tu walioweza kufanya hivyo kutokana na wengi kuogopa watakuwa wanahamia katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

Shehena ya chakula cha msaada  kilichopangwa kugawiwa katika maeneo kadhaa ya mji huo inaelekea kumalizika baada ya mashirika ya kimataifa ya misaada ya kiutu na washirika wao nchini humo kuthibitisha kugawa chakula hicho katika siku za hivi karibuni. Hakuna misaada ya kiutu iliyopelekwa katika maeneo ya jirani mashariki ya mji huo tangu wakati  ulipozingirwa na vikosi vya serikali Julai mwaka huu.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe

Mhariri: Grace Patricia Kabogo