Mashahidi: Trump alimshinikiza Pence kubatilisha matokeo
17 Juni 2022Ushahidi huo umetolewa na wasaidizi wa karibu wa makamu wa rais wa zamani wa Marekani Mike Pence katika duru ya tatu ya uchunguzi wa wazi unaofanywa na Bunge la Marekani kuhusu mkasa wa kuvamiwa kwa majengo ya bunge mnamo Januari 6 mwaka jana.
Kamati inayochunguza kisa hicho imefafanua jinsi Trump alivyomtia kishindo Pence akimtaka kubadili matokeo ya uchaguzi licha ya kuarifiwa mara kadhaa kwamba kufanya hivyo ni kinyume na sheria.
Marc Short, aliyekuwa mkuu wa utumishi wa ofisi ya makamu wa rais amesema kupitia ushuhuda kwa njia ya video kuwa Pence alimwarifu mara nyingiTrump kwamba haiwezekani kusitisha kura ya kumuidhinisha Joe Biden kuwa rais.
Hata hivyo inaarifiwa Trump aliendelea kumshinikiza Pence kutafuta njia za kuyakataa matokeo na ikiwezekana kutumia nafasi yake ya rais wa Baraza la Seneti kuzuia kura ya kumuidhinisha Biden. Ushahidi sawa na huo umetolewa pia na mwanasheria wa Pence, Gregory Jacob.
Kamati: Trump alitaka Pence kuvunja katiba
Kamati ya bunge inatumia ushuhuda huo kuonesha kwamba shinikizo hilo la Trump kwa Pence lilikuwa msingi wa kiongozi huyo kutaka kubakia madarakani kinyume na katiba baada ya kushindwa uchaguzi.
Kadhalika kamati inalenga kudhihirisha kuwa msukumo huo wa Trump ndiyo ulichangia pakubwa wafuasi wa kiongozi huyo kuitikia miito ya kuyavamia majengo ya bunge kuzuia upigaji kura baada ya Pence kukataa kumtii Trump.
"Donald Trump alitaka Mike Pence afanye kitu ambacho hakuna makamu wa rais yeyote aliyewahi kukifanya: rais huyo wa zamani alimtaka Pence kukataa kura au kumtangaza yeye Trump kuwa mshindi au kura zirejeshwe kwenye majimbo zikahesabiwe tena" amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge, Bennie Thompson .
Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo Liz Cheney amemtuhumu mwanasheria wa Trump, John Eastman kuwa msanifu mkuu wa kile alichokitaja kama"njama isiyoingia akilini" ya kubadili matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 huku akifahamu kwamba kumsaidia Trump kufanya hivyo ni kinyume na sheria.
Mashuhuda wazungumzia maneno ya kejeli ya Trump kwa Pence
Katika ushahidi huo wako waliosema shinikizo lilikuwa kubwa kiasi wakati mwingine Trump alitumia maneno ya dhihaka na ukali kumkabili Pence alipoonesha kukataa wito wa kubatilisha matokeo.
Imearifiwa Trump alimpachika majina Pence, akimwita "dhaifu na asiye na ushujaa wa kubadili matokeo ya uchaguzi".
Alipokuwa kwenye mkutano na kundi la wafuasi wake mjini Washington muda mfupi kabla ya kuvamiwa majengo ya bunge Trump aliwataka wafuasi wake wapigane "kufa na kupona" akisema makamu wake asingeweza kuzuia Biden kuidhinishwa kuwa rais.
Baadhi ya viongozi wa kamati ya bunge ya uchunguzi wamesema ushahidi uliopo unaonesha Trump alikuwa tayari hata "kumtoa kafara" makamu wake ili asalie madarakani.
Trump aliamua kutumia njia za kumshinikiza Pence kubatilisha ushindi wa Biden baada ya majaribio yake kadhaa ya kisheria ya kupinga matokeo ya uchaguzi kuambulia patupu.