1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashabiki waruhusiwa tena viwanjani Bundesliga

4 Aprili 2022

Mechi za duru ya 28 ya msimu huu wa Bundesliga zilikuwa za aina yake. Mashabiki waliruhusiwa kurejea katika viwanja vya Ujerumani – Bundesliga baada ya kuondolewa vizuizi vya corona.

https://p.dw.com/p/49RoL
Fuflball: Bundesliga I Borussia Dortmund - RB Leipzig
Picha: Martin Meissner/AP/picture alliance

Katika dimba la Westfalenstadion, ilitarajiwa kuwa ni usiku wa furaha na sherehe kwa Borussia Dortmund wakati waliwakaribisha uwanjani mashabiki 81,365. Badala yake, timu hiyo ya kocha Marco Rose ilibutuliwa na RB Leipzig kwa mabao manne kwa moja na kuwaacha Dortmund midomo wazi. Na baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, baadhi ya mashabiki wakawazoea wachezaji wa Dortmund, na wengine wakimtaka kocha Rose aondoke. Hiyo inaonyesha kuwa matatizo ya BVB ni ya zamani Zaidi kuliko hata janga la corona. Msikilize kocha Rose "Kimsingi inauma sana, sana, inasikitisha sana kwa sababu tulikuwa tumepanga mengi, na tulikuwa tumetazamia kuwaona mashabiki wetu, ambao kila mtu angeweza kuwa hapa tena. Nadhani tulicheza dakika 20 za kwanza vizuri, tukatawala mchezo na kuwabana Leipzig. Kisha tukafanya makosa na kushindwa kufunga bao la kwanza. Na Leipzig ni timu ambayo ni hatari kweli na hilo lilidhihirika katika mechi ya leo"

Fuflball: Bundesliga I Borussia Dortmund - RB Leipzig
Leipzig waliwaduwaza Dortmund nyumbani kwaoPicha: Dennis Ewert/RHR-Foto/IMAGO

Na kwa matokeo hayo, ni kama ndio mbio wa ubingwa wa msimu huu zimekamilika. Bayern tayari walikuwa wamewapiga Freiburg 4-1. Kama Bayern na Dortmund watashinda mechi zao mbili zijazo, miamba hao wa Bavaria huenda wakabeba ubingwa wao wa kumi mfululizo kwa kuwazaba Dortmund wakati watakapokutana mjini Munich mnamo Aprili 23.

Lakini kuna tukio la kushangaza lililoigubika mechi ya Freiburg na Bayern. Ambapo Bayern ilicheza na wachezaji 12 uwanjani kwa sekunde kadhaa kabla ya kugundulika. Katika dakika ya 86 wakati Bayern ikiwa kifua mbele 4 – 1, walitaka kufanya mabadiliko kwa kuwaingiza Marcel Sabitzer na Niklas Sule na kuwatoa Kingsley Coman na Corentin Tolisso. Lakini Coman akabaki uwanjani. Kwa sababu ubao ulionyesha namba yake za zamani na sio anayovaa sasa kwenye jezi. kocha wa Bayern Julian Nagelsmann alisema mkanganyiko huo ni wa kushangaza sana "Ni hali ya kushangaza, bila shaka hatupaswi kuizungumzia na naweza pia kuelewa kuwa mashabiki wamekasirishwa nayo na sio vinginevyo, na bila shaka ni rahisi kuizungumzia kwa mtizamo wangu kuliko mtizamo wa Christian, lakini sidhani kama katika wakati huu wa mchezo hali hiyo ingebadilisha matokeo. Tulikuwa tunaongoza 3-1 kwa wakati huo

Naye kocha wa Freiburg Christian Streich anasemaje? "Ninaamini kabisa kuwa hatupaswi kuwasilisha malalamiko. Lakini zipo sheria kuhusu hilo. Lazima kuwepo na sheria ya tukio kama hilo na kama kuna sheria basi itatumika na tutafuata sheria hiyo."

Fußball: Bundesliga I SC Freiburg - Bayern München
Bayern ilicheza na wachezaji 12 kwa sekunde kadhaaPicha: Philipp von Ditfurth/dpa/picture alliance

Msemaji wa chama cha kandanda Ujerumani DFB amesema Freiburg ina hadi leo usiku kuamua kama wanataka kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo hayo. Hakuna hatua itakayochukuliwa na DFB kama Freiburg itaamua kusalia kimya.

Nambari tatu Bayer Leverkusen iliharibu siku ya kwanza kazini ya kocha Felix Magath kwa kuilaza Hertha 2 – 1. Kichapo hicho kimeiweka Hertha katika nafasi ya pili kutoka mkiani. Gladbach ilitoka sare ya 1-1 na Mainz. Gladbach wako nafasi ya 12 pointi nne nyuma ya Mainz.

Katika vita vya kushuka daraja, Augsburg waliondoa katika nafasi tatu za mkia kwa ushindi wa 3- 0 dhidi ya Wolfsburg. Ushindi huo unainyanyua Augsburg hadi nafasi ya 14. Msikilize mchezaji wa Wolfsburg Lukas Nmecha "Kuruhusu bao kama lile baada ya dakika chache inatia uchungu lakini tulikuwa na nafasi za kupambana na kujiondoa katika hali hiyo na tungeshinda mchezo huo lakini tukafanya makosa mengi na kwa jumla hatukuwa vizuri sana.

Arminia Bielefeld ilitoka sare ya 1 -1 na Stuttgart. Kumaanisha Hertha, Bielefeled na Augsburg zote ziko nyuma ya Stuttgart na pengo la pointi moja tu. Bochum ilishinda 2 – 0 kwa Hoffenheim na washika mkia Greuther Furth wakatoka sare tasa na Eintracht Frankfurt.

afp, reuters, dpa, ap