Marudio ya uchaguzi Liberia yasitishwa
1 Novemba 2017Mahakama hiyo ya Juu ilisema Jumatano kwamba wawakilishi wa tume ya kusimamia uchaguzi nchini humo na wale waliowasilisha rufaa wafike mahakamani Alhamis.
Mgombea aliyemaliza katika nafasi ya tatu kwenye uchaguzi uliopita Charles Brumskine kupitia chama chake cha Liberty, ndiye aliyewasilisha rufaa hiyo mahakamani baada ya uchaguzi wa mwezi uliopita ambao haukutoa mshindi wa moja kwa moja na hivyo kupelekea duru ya pili iliyokuwa imepangwa kufanyika Novemba 7 kati ya gwiji wa soka wa zamani George Weah na makamu wa rais Joseph Boakai.
Katika agizo lililotolewa Jumatano, mahakama imekiagiza chama cha Liberty pamoja na tume ya kusimamia uchaguzi huko Liberia kuandikisha taarifa kufikia kesho, lakini bado haijabainika iwapo mahakama hiyo itatoa uamuzi wake kabla Novemba 7.
Chama cha Boakai kiliunga mkono rufaa hiyo
Mwenyekiti wa chama cha Liberty Bejamin Sanvee baada ya uamuzi huo alisema, "hii ni hatua kubwa ya kuelekea kuzuri, nashukuru mahakama imetambua uzito wa masuala haya," alisema Sanvee, "na imechukua hatua kwa ajili ya kutetea sheria na demokrasia," aliongeza mkuu huyo.
Mapema wiki hii, chama tawala cha Boakai kilitangaza kwamba kinaunga mkono rufaa hiyo. Kilimtuhumu rais Ellen Johnson Sirleaf ambaye ni mwanachama wao, kwa kuingilia uchaguzi wa Oktoba tarehe 10 kwa kufanya mikutano ya siri na mahakimu wa uchaguzi.
Sirleaf ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi na mbili iliyopita amekanusha kuwa mikutano hiyo ilikuwa haifai. Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wakiwemo kutoka Umoja wa Ulaya na kituo cha Carter wamesema hawakuona matatizo yoyote katika raundi ya kwanza ya kura.
Uamuzi wa mahakama hiyo unaonesha jukumu muhimu la mahakama Afrika katika masuala ya usimamizi wa uchaguzi. Mahakama ya Kenya ilifutilia mbali uchaguzi wa Agosti nchini humo, ingawa uchaguzi mpya uliofanywa wiki iliyopita ulishuhudia upinzani ukigoma kushiriki.
George Weah alishinda duru ya kwanza kwa zaidi ya asilimia 38
Katika mji Mkuu wa Liberia, Monrovia Jumatano, polisi wa kupambana na ghasia walikuwa wameweka ulinzi nje ya Mahakama ya Juu wakati ambapo uongozi umewataka wananchi kusalia watulivu.
Sam Collins, msemaji wa polisi kupitia kituo kimoja cha redio huko Liberia amewaambia wananchi wasitaharuki na kwamba wanaweza kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
George Weah alishinda duru ya kwanza ya uchaguzi huo kwa kupata asilimia 38.4 ya kura zilizopigwa huku mpinzani wake Boakai akipata asilimia 28.8. Wiki iliyopita Weah aliungwa mkono na mbabe wa zamani wa kivita nchini humo Prince Johnson aliyepata asilimia 8 ya kura katika raundi ya kwanza ya kura.
Afisa mmoja mkuu kutoka chama cha Weah cha CDC Morluba Morlu amesema bado anatarajia marudio hayo ya uchaguzi kufanyika wiki ijayo.
Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga