Marekani yazingirwa na virusi wakati ikisherehekea uhuru
4 Julai 2020Wakati fukwe zimefungwa kutoka eneo moja la pwani hadi jingine na maafisa wakiwataka Wamarekani kubakia majumbani mwao, hali isiyokuwa ya furaha kuelekea katika kile ambacho kwa kawaida ni mwishoni mwa juma kunakochomwa nyama na hali ya hewa ya jua imelemea mapambano ya kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 katika kitovu cha janga hilo duniani.
"Ni idadi usiyoweza kuamini," amesema Faisal Masud , mkurugenzi wa matibabu katika hospitali ya Methodist mjini Texas, ambayo maafisa wamesema inakaribia kabisa kuzidiwa na wagonjwa.
Ukigusa karibu kila nchi duniani tangu kujitokeza nchini China mwishoni mwa mwaka jana, virusi vya corona vimewaambukiza kiasi ya watu milioni 10.9 na kuwauwa watu 522,000 duniani, na kuzima uchumi uliokuwa hapo kabla ukikua kwa kasi na kusababisha maisha ya watu kuzimika.
Lakini wakati Ulaya na sehemu nyingi za Asia kwa kiasi kikubwa zimeweza kudhibiti virusi hivyo vya corona , kwa kiasi kikubwa Uingereza inajitayarisha kufungua biashara zake, mikahawa na cinema, lakini nchini Marekani ugonjwa huo umewauwa karibu watu 130,000 huku kukiwa na ongezeko kubwa la kesi mpya za maambukizi ambapo mtaalamu wa ngazi ya juu wa magonjwa ya kuambukiza Anthony Fauci amesema "unaiweka nchi nzima katika hatari."
Rekodi ya maambukizi
Nchi hiyo yenye uchumi mkubwa duniani imevunja rekodi yake ya maambukizi mapya kwa siku ya tatu mfululizo hadi jana Ijumaa, kwa kuwa na zaidi ya maambukizi 57,000 katika muda wa masaa 24. Inatarajiwa kufikisha maambukizi milioni tatu wiki ijayo, ambapo kesi zinaongezeka hususan upande wa kusini na magharibi.
Rais wa Marekani Donald Trump , akiwa katika eneo la Mount Rushmore kwa ajili ya sherehe za kurusha fashifashi pamoja na maelfu ya wahudhuriaji wakikaribiana na barakoa si lazima, hadi sasa amepuuzia ongezeko hilo la maambukizi mapya.
Lakini mtangulizi wake Barack Obama amewataka Wamarekani kujiweka "salama na kuwa wajanja."
"Itatulazimu kuchukua hatua kwa pamoja kudhibiti virusi hivi. kwa hiyo vaa barakoa. Safisha mikono yako. Na wasikilize wataalamu , sio watu ambao wanajaribu kutugawa," aliandika katika ukurasa wa Twitter.
Shirika la afya ulimwenguni WHO limezitaka nchi ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa , "kuamka" na kuona hali halisi.
"Watu wanapaswa kuamka. Data hazidanganyi, " mkurugenzi wa masuala ya dharura wa WHO Michael Ryan aliwaambia waandishi habari mjini Geneva.