Marekani yazikosoa nchi za Sahel kushindwa kurejesha utulivu
17 Desemba 2019Marekani imezikosoa nchi za Afrika Magharibi za ukanda wa Sahel jana Jumatatu, ikisema viongozi wake wameshindwa kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha utulivu, wakati mashambulizi ya wanajihadi yakiongezeka.
Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Cherith Norman alilieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuwa kunahitajika uwajibikaji zaidi katika kukabiliana na machafuko ya kikanda kutoka kwa serikali za nchi hizo.
Aidha alisema mara kadhaa jeshi linashindwa kushughulikia chanzo cha mizozo, na kuongeza kwamba Marekani imeidhinisha msaada wa zaidi ya Dola bilioni 3.5 mwaka 2017 na 2018 ili kuunga mkono uthabiti na usalama wa muda mrefu katika eneo la Afrika Magharibi.
Wiki iliyopita mamia ya wapiganaji waliishambulia kambi ya jeshi huko Niger na kuwaua watu 71, ikiwa ni shambulio baya tangu ghasia za wanapiganaji wa Kiislamu walio na misimamo mikali zilipoanza kutoka nchi jirani ya Mali mwaka 2015.