Marekani yawatuhumu mawaziri wa Urusi kwa unyama Ukraine
24 Februari 2023Yellen ameyasema haya katika mkutano wa kilele wa nchi 20 zilizostawi na zinazoinukia kiuchumi G20, huku mwenyeji wa mkutano huo India ikikwepa kuutaja mzozo huo uliodumu kwa mwaka mmoja sasa katika hotuba ya ufunguzi.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, bila kuvitaja moja kwa moja vita vya Ukraine, ametoa wito kwa mawaziri hao wa fedha kuwatazama zaidi watu wanaoteseka duniani.
Usalama wa chakula na nishati vyatia hofu duniani
Modi amesema janga la Uviko 19 na ongezeko la mivutano ya kikanda na kisiasa katika sehemu tofauti duniani ni mambo yaliyopelekea baadhi ya nchi kufikia kiwango cha madeni wasichoweza kukidhibiti, kutatizwa kwa mifumo ya usambazaji wa bidhaa na kitisho kwa usalama wa chakula na nishati.
"Usalama wa chakula na nishati yamekuwa mambo yanayoleta hofu kote duniani. Hata uwezo wa kifedha wa nchi nyingi unatishiwa na kiwango cha madeni. Imani kwa taasisi za kifedha za kimataifa imeondoka na hii ni kwasababu taasisi hizi zimechukua muda mrefu kubadilika," alisema Modi.
Naye waziri Yellen ametoa wito kwa nchi za G20 kuongeza juhudi za kuiunga mkono Ukraine na kuudhibiti uwezo wa Urusi kuendeleza vita.
Yellen amesema anatarajia kuona Urusi ikilaaniwa katika mkutano huo kutokana na uvamizi wake na uharibifu iliyosababisha kwa Ukraine na uchumi wa dunia.
India ambayo inashikilia urais wa zamu wa G20 haitaki kuwepo na mjadala wa vikwazo zaidi kwa Urusi na inajitahidi kutotumia neno "vita" katika mawasiliano yake kwenye mkutano huo.
Uchumi wa dunia haupo pabaya vile sasa
Mkutano huu unafanyika wakati ambapo kuna dalili nzuri kuhusiana na uchumi wa dunia ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika mkutano uliopita, ambapo chumi za nchi kadhaa zilikuwa zinaelekea kuanguka kufuatia ongezeko la bei za nishati na chakula zilizosababishwa na vita hivyo vya Ukraine.
Mkutano huo wa G20 pia unatarajiwa kufanya mazungumzo kuhusiana na kusamehewa madeni kwa nchi zilizoathirika zaidi huku shinikizo likielekezwa zaidi kwa China ambayo ndiyo nchi inayotoa mikopo kwa kiasi kikubwa duniani pamoja na nchi zengine.
Katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya video, waziri wa fedha wa China Liu Kun, kwa mara nyengine ameusisitiza msimamo wa China kwamba Benki ya Dunia na benki zengine zishiriki hatua hiyo ya kupunguza madeni kwa baadhi ya nchi zilizolemewa.
Kundi la G20 linajumuisha nchi zilizo katika kundi la G7 pia kama Urusi, China, India, Brazil na Saudi Arabia, ingawa waziri wa fedha wa Urusi Anton Siluanov na gavana wa benki kuu Elvira Nabiullina hawakuwepo katika mkutano huo nchini India. Urusi imewakilishwa na manaibu wao.
Chanzo: Reuters