Marekani yatangaza mazungumzo ya kusitisha mapigano Sudan
24 Julai 2024Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema mjini Washington kuwa amelialika jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF kushiriki mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Marekani kuanzia Agosti 14.
Soma pia: Pande zinazovutana kwenye mzozo wa Sudan zaanza mazungumzo, Geneva
Kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, ambaye amekuwa vitani na jeshi linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan kwa karibu mwaka mmoja, ameukaribisha mwaliko wa Blinken na akathibitisha kuwa upande wake utashiriki katika mazungumzo hayo. Ameyasema hayo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X.
Soma pia: Marekani yatoa nyongeza ya mamilioni ya dola kuisaidia Sudan
Mazungumzo ya awali mjini Jeddah, Saudi Arabia, yalishindwa kusitisha mapigano ambayo yamesababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao, na yakaufanya mji mkuu Khartoum kubakia magofu. Juhudi zilizofuata za upatanishi, zikiwemo za Umoja wa Afrika, zimeshindwa kuzileta pamoja pande zinazohasimiana kwenye chumba kimoja, huku watalaamu wakisema vikosi vyote viwili vya kijeshi vinapambania udhibiti nchini Sudan. Mazungumzo hayo ya Uswisi yatakayosimamiwa na Marekani yataongozwa kwa pamoja na Saudia na yatajumuisha wajumbe kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Umoja wa Mataifa kama waangalizi.