Marekani kurejesha utoaji wa misaada ya chakula Ethiopia
15 Novemba 2023Marekani imetangaza kurejesha utoaji wa msaada wa chakula nchini Ethiopia, baada ya serikali kukubali kuruhusu misaada hiyo kufuatiliwa. Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani USAID, limetangaza kuanza upya utoaji wa chakula mwezi ujao kwa muda wa mwaka mmoja kwanza ili kuthibitisha kama serikali inatimiza ahadi zake.
Shirika hilo lilisitisha utoaji wa misaada yote ya chakula nchini Ethiopiamnamo mwezi Juni, baada ya kuwepo na ripoti za hujuma iliyoratibiwa ya kubadilisha njia ya usambazaji wa msaada wa chakula ili usiwafikie wenye mahitaji.
Marekani haikuwataja hadharani wahusika lakini mashirika ya misaada yalizilaumu pande zote, za mamlaka ya shirikisho na ya kikanda, huku wanajeshi wakinufaika kutokana na mauzo ya vyakula vilivyotolewa. Marekani imeikosoa vikali Ethiopia, dhidi ya kampeni yake ya kijeshi ya miaka miwili katika mkoa wa Tigray.