Marekani yasema hatua zimepigwa katika mazungumzo ya Gaza
24 Agosti 2024Ikulu ya White House imesema mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani - CIA William Burns alikuwa miongoni mwa maafisa wa Marekani walioshiriki katika mazungumzo ya Cairo, akiungana na wakuu wa shirika la ujasusi la Misri na la usalama wa taifa.
Soma pia: Israel yawasili Cairo kwa mazungumzo ya vita vya Gaza
Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Kirby amesema mafanikio yamepatikana, na kinachohitajika kutoka kwa pande zote ni kuungana na kufanya kazi ya utekelezaji wa makubaliano hayo. Hayo yalijiri wakati mapigano yakipamba moto jana, huku mashuhuda wakiripoti makabiliano makali kaskazini, na kusini mwa Gaza.
Wakati huo huo, Hamas imemlaumu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kukataa kufikia mapatano ya kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, kwa kuja na madai mapya ya kutaka jeshi la Israel ndilo lipewe udhibiti usio ukomo wa mpaka kati ya Ukanda huo na Misri. Msemaji wa Netanyahu ameeleza kuwa tayari ujumbe wa Israel upo nchini Misri kuzungumzia juu ya kusimamisha mapigano na kuachiwa kwa mateka. Hata hivyo, wawakilishi wa Hamas hawashiriki.