Marekani yajitayarisha tena na kimbunga Nate
7 Oktoba 2017Watabiri wa hali ya hewa wamesema upepo huo mkali na mvua huenda ukafika katika pwani ya ghuba ya Marekani kama kimbunga mwishoni mwa juma.
Maafisa wa Louisiana na Mississippe wametangaza hali ya hatari na Louisiana wameamru baadhi ya watu waondolewe katika maeneo ya pwani na visiwa vya vizuwizi kabla ya kutarajiwa kuwasili kwa kimbunga hicho leo Jumamosi usiku ama mapema Jumapili. Uondoaji wa watu ulianza katika maeneo ya nje baharini katika maeneo yanayochimbwa mafuta katika eneo hilo la ghuba.
Serikali ya jimbo la Mississippi imesema itafungua vituo 11 vya kuhifadhi watu katika maeneo nje ya eneo la karibu la pwani, ambapo mabasi yametayarishwa kwa ajili ya watu ambao hawana magari.
Kituo kinachohusika na masuala ya vimbunga nchini Marekani kimeonya kwamba kimbunga Nate kinaweza kupandisha viwango vya bahari kwa zaidi ya futi nne hadi saba , mita 1.2 hadi mita 2.1 , kutoka mji wa Morgab, Louisiana , hadi mpaka kati ya Alabama na florida. Kimbunga hicho tayari kimesababisha mafuriko makubwa katika eneo kubwa la Amerika ya kati.
Kituo hicho kimeongeza mji wa New Orleans na ziwa Pontchartrain katika orodha ya hivi karibuni kabisa ya tahadhari kwa kimbunga hicho.
Kimbunga kinaongezeka nguvu na kasi
Kimbunga hicho ambacho kina wastani wa upepo unaokwenda kasi ya kilometa 65 kwa saa ilipofika jana Ijumaa mchana na huenda kikaongezeka nguvu wakati kikiwa katika eneo la bahari la kaskazini magharibi la visiwa vya Karibiki kabla ya kuingia katika eneo la Cancun mwishoni mwa rasi ya Yucatan nchini Mexico. Inaweza kulikumba eneo la ghuba ya pwani ya Marekani karibu na New Orleans.
Kimbunga hicho kilionekana kiasi ya kilometa 145 kaskazini mashariki mwa mji wa kitalii nchini Mexico wa Cozumel na kuongeza kasi kuelekea upande wa kaskazini na kaskazini magharibi hadi kilometa 35 kwa saa. Maafisa walifuta masomo kwa wanafunzi siku ya Ijumaa mchana katika maeneo ya jimbo la pwani ya Karibiki katika jimbo la Quintana Roo, ambako Cozumel na Cancun zinapatikana.
Gavana Carlos Joaquin amesema inaonekana kwamba kimbunga hicho kitabakia nje ya pwani na hakitashambulia eneo la ndani , na kuongeza , kwamba , "naamini , ni habari nzuri."
Shule zilifungwa Nicaragua
Nchini Nicaragua , kuwasili kwa kimbunga Nate kunafuatia wiki mbili za mvua ambayo ilikuwa inanyesha karibu wakati wote ambayo imeacha ardhi ikiwa na maji mengi na mito kujaa maji. Maafisa wameiweka nchi yote katika hali ya tahadhari na kuonya kwamba mafuriko na maporomoko ya ardhi huenda yakatokea.
Makamu wa rais wa Nicaragua na msemaji wake, Rosario Murillo, wamesema kwamba kiasi watu 11 wamefariki nchini humo kutokana na kimbunga hicho. Mapema siku ya Alhamis alisema watu 15 wamefariki kabla na baadaye kubadilisha na kusema baadhi yao wanahesabiwa kwamba hawajulikani waliko.
Hakutoa maeneo zaidi kuhusu vifo vyote, lakini amesema wanawake wawili na mwanamume mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi katika wizara ya afya walichukuliwa na mafuriko katika mrefeji uliojaa maji katika mji wa kati wa Juagalpa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Lilian Mtono