1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaishambulia Syria kwa makombora

Sylvia Mwehozi
7 Aprili 2017

Marekani imerusha makombora kadhaa ya kasi katika moja ya kambi ya jeshi la anga nchini Syria, sehemu ambayo inadai kwamba shambulio la silaha za sumu lilirushwa kutokea hapo mapema wiki hii.

https://p.dw.com/p/2aqdK
Syrien US-Angriff auf Luftwaffenbasis Al-Schairat
Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/M. Voskresenskiy

Meli mbili za kivita za Marekani zimerusha makombora takribani 59 ya kasi kutoka mashariki mwa bahari ya Meditrania katika kambi ya jeshi la anga la Syria inayodhibitiwa na vikosi vya serikali ya Rais Bashar Al-Assad ikiwa ni hatua ya kulipiza shambulio la gesi ya sumu lililolengwa katika maeneo ya waasi siku ya Jumanne.

Akiwa anakabiliwa na mgogoro mkubwa wa sera yake ya nje tangu kushika madaraka Januari 20, Rais Donald Trump amechukua maamuzi magumu na ya moja kwa moja katika mzozo wa vita uliotimiza miaka sita, na kuibua hatari ya kuvaana uso kwa uso na Urusi na Iran walio washirika wakuu wa kijeshi wa Assad.

Maafisa wa Marekani wanadai kwamba waliviarifu vikosi vya Urusi kabla ya kutekeleza mashambulizi hayo ya makombora na kujizuia kuvipiga vikosi vya Urusi vilivyoko katika ngome hiyo.

Trump aidhinisha shambulio

Syrien USA Luftangriff auf Militärbasis
Meli ya kivita ya Marekani katika bahari ya Meditrenia Picha: picture-alliance/AP Photo/US Navy/F. Williams

Rais Trump ametangaza kuidhinisha shambulio hilo akiwa jimboni Florida alipokuwa anakutana na rais wa China Xi Jinping, "usiku huu nimeamuru mashambulizi ya kijeshi katika eneo la kambi ya anga Syria, sehemu ambayo shambulio la silaha za kemikali lilitekelezwa. Ni katika umuhimu wa maslahi ya usalama wa taifa wa Marekani kuzuia kuenea kwa matumizi ya umwagaji damu ya kemikali," amesema Rais Trump.

Trump aliamuru mashambulizi hayo siku moja baada ya kumshutumu Assad kwa shambulio la wiki hii la kemikali ambalo limewaua watu zaidi ya 70 wengi wao wakiwa watoto katika mji wa Khan Sheikhoun. Hata hivyo serikali ya Syria imekanusha kufanya shambulio hilo.

Makombora hayo yamekilenga kituo cha anga cha Shayrat na kupiga uwanja wa ndege, ndege na vituo vya mafuta. Shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini humo limesema askari wanne wa Syria wameuliwa katika shambulio hilo ambalo linaelezwa limeiharibu ngome hiyo kwa kiasi kikubwa.

Urusi na Iran zalaani shambulio 

Syrien Idlib Giftgasangriff
Mtoto wa Syria aliyeathirika na kemikali za sumuPicha: picture-alliance/abaca/S. Zaidan

Rais wa Urusi Vladmir Putin anaamini mashambulizi hayo ya makombora katika kambi ya anga ya Syria yamevunja sheria za kimataifa na yamevuruga pakubwa mahusiano ya Marekani na Urusi, kama alivyonukuliwa na mashirika ya habari.

Kiongozi huyo amekiita kitendo hicho kuwa ni "uchokozi dhidi ya taifa huru" kutokana na taarifa za kutungwa katika jitihada za kuisahaulisha dunia juu ya mauaji ya raia huko Iraq, kwa mujibu wa msemaji wa Putin, Dmitry Peskov.

Iran ambaye ni mshirika mkuu wa Rais Assad imelaani shambulio hilo ikisema kitendo hicho ni cha hatari, uharibifu na uvunjifu wa sheria za kimataifa.

Israel kwa upande wake imeupongeza uamuzi huo ikisema ni ujumbe tosha kutoka kwa Trump kwamba matumizi na usambazaji wa silaha za kemikali havitavumiliwa.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo katika mkutano wa faragha kujadili shambulio hilo la Marekani.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Josephat Charo