1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaidhinisha dawa ya Ebola kutibu COVID-19

2 Mei 2020

Marekani imeidhinisha dawa ya majaribio kutumiwa kwa dharura kutibu wenye maambukizi ya virusi vya Corona.Dawa hiyo ilitengenezwa kutibu ugonjwa wa mripuko wa Ebola uliozikumba nchi za Afrika

https://p.dw.com/p/3bgdV
Remdesivir antivirales Medikament in Erprobung
Picha: AFP/U. Perrey

Marekani imeidhinisha dawa ya majaribio kutumiwa kwa dharura kutibu wenye maambukizi ya virusi vya Corona wakati majimbo mengi ya Marekani yakianza kuondowa vizuizi vya kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo licha ya kuonekana kuwepo ongezeko jingine la vifo kutokana na ugonjwa huo.

Kuidhinishwa kwa dawa hiyo ni hatua ya karibuni katika juhudi za ulimwengu za kujaribu kutafuta tiba mwafaka na chanjo ya virusi hivyo,vilivyosababisha nusu ya idadi ya watu duniani kukaa majumbani huku pia uchumi wa dunia ukipata pigo na  watu milioni 3.3 kupata maambukizi.

Dawa hiyo dhidi ya virusi inayoitwa Remdesivir awali ilitengenezwa kutibu maradhi ya Ebola, imeruhusiwa ijumaa kuanza kutumika baada ya kufanyika majaribio makubwa yaliyobaini kwamba inasaidia katika uponyaji kwa wagonjwa wa Covid-19 wenye hali mbaya.

Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Ijumaa akizungumza akiwa ikulu ya White House alikokutana na Daniel O'Day, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya utafiti wa kisayansi na utengenezaji wa madawa ya Gilead Sciences, iliyotengeneza dawa hiyo ya Remdesivir, alisema ni hatua inayoleta matumaini. Dawa hiyo inafanya kazi kwa kuzuia kuongezeka kwa kiwango cha virusi ndani ya mwili wa mgonjwa. Kuidhinishwa kwake kumekuja katika wakati ambapo viongozi wa Marekani wanapambana na hali ya kuongezeka kwa shinikizo la wananchi waliochoshwa na vizuizi vya kuwataka wabakie majumbani.

USA Washington | Coronavirus | Donald Trump zu Remdesivir, Medikament
Picha: picture-alliance/Zuma/SMG

Marekani ina visa kiasi milioni 1.1 vya maambukizi vilivyothibitishwa na takriban vifo 65,000 hali inayoifanya nchi hiyo kuwa nchi yenye idadi kubwa kabisa ya waathirika kuliko nchi nyingine yoyote duniani na rais Donald Trump anajaribu kutafuta njia za kuibadili hali hiyo,huku taifa hilo lenye uchumi mkubwa duniani likikabiliwa na mamilioni ya watu walioachwa bila ajira.

Trump amesema anataraji kwamba watafanikiwa kupunguza idadi ya wanaokufa kufikia chini ya 100,000 ambayo ni idadi ya kutisha, ingawa mwanzoni mwa wiki hii rais huyo alisema huenda nchi yake ikatarajia vifo 60,000 au 70,000. Texas ni jimbo kubwa la Marekani ambalo bado limeamua kutoondowa vizuizui  huku wanaopinga vizuizi hivyo wakijitokeza kuandamana katika majimbo mengi ya Marekani ikiwemo Carlifonia. Katika jimbo hilo la Carlifornia maafisa walizifunga tena fukwe za kuogelea kuanzia siku ya Ijumaa ili kuzuia kujirudia tena matukio yaliyoshuhudiwa wikendi iliyopita pale umati wa watu ulipomiminika kwenye fukwe hizo.

Serikali mbali mbali duniani zinapambana kupima kishindo cha kisiasa na shinikizo la kiuchumi katika kuondowa vizuizi hivyo huku ikiwepo haja ya kuchukuliwa hatua ya afya ya umma dhidi ya kusambaa  kwa virusi hivyo. Nchi nyingi za Ulaya zimeanza kuondowa vizuizi ambapo mamlaka katika baadhi ya nchi zilizoathirika zaidi kama vile Uhispania zikiripoti ishara kwamba janga hilo linaanza kupungua   

     

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Amina Mjahid

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW