1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Asili na mazingiraUmoja wa Falme za Kiarabu

Marekani yaahidi dola bilioni tatu kwa mfuko wa mazingira

Saleh Mwanamilongo
2 Desemba 2023

Kamala Harris aliuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa COP28 Jumamosi kwamba Marekani itachangia dola bilioni 3 kwa mfuko wa mabadiliko ya tabia nchi duniani.

https://p.dw.com/p/4Zhyc
VAE Dubai COP28 | Übersicht
Picha: Wang Dongzhen/Xinhua/IMAGO

Kamala Harris aliwambia viongozi na wajumbe kwenye mkutano huo wa Dubai kwamba Marekani inaonyesha kwa vitendo jinsi ulimwengu unavyoweza na kwa lazima kukabiliana na shida hii ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kiwango hicho kipya cha fedha ambacho lazima kiidhinishwe na Bunge la Marekani, kitaingia katika Mfuko wa kukabiliana na madhila ya mabadiliki ya tabia nchi duniani kwa kifupi,(GCF), ambao uliundwa mwaka wa 2010.

Mchango wa mwisho wa Marekani katika mfuko huo wa mataifa  hiyo yanazoendelea ulitolewa chini ya Rais wa wakati huo Barack Obama, ambaye alitoa dola bilioni 3 mwaka 2014.

Ahadi za nchi zilizoendelea

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amemuakilisha rais Biden kwenye mkutano wa Dubai
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amemuakilisha rais Biden kwenye mkutano wa DubaiPicha: Amr Alfiky/REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden alimtuma Harris badala yake kwenye mkutano huo wa COP28. Mfuko mkubwa zaidi wa hali ya hewa duniani hutoa misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika nchi zinazoendelea, kama vile nyenzo za nishati ya  jua nchini Pakistan au usaidizi katika uratibu wa mafuriko nchini Haiti.

Kabla ya tangazo hilo la Marekani, dola bilioni 13.5 zilikuwa zimeahidiwa kwa mfuko huo wa GCF. Kushindwa kwa mataifa tajiri kutimiza ahadi za kifedha kusaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kumechochea mivutano na kutoaminiana katika mazungumzo ya Dubai.

Nchi zinazoendelea ambazo hazijahusika sana na uchafuzi wa mazingira zinatafuta usaidizi kutoka kwa mataifa tajiri zaidi yanayochafua mazingira ili kukabiliana na athari zinazozidi kuwa mbaya na za gharama kubwa za hali mbaya ya hewa, na kwa mabadiliko yao hadi vyanzo safi vya nishati.

Mwito wa Papa Francis kuachana na nishati ya visukuku

Papa Francis awarai viongozi wa dunia kufikia mafanikio yakuokoa sayari
Papa Francis awarai viongozi wa dunia kufikia mafanikio yakuokoa sayariPicha: Peter Dejong/AP/dpa/picture alliance

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis alitoa wito Jumamosi kwa viongozi katika mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP28 huko Dubai kujitokeza na kufikia "mafanikio" ya kuokoa sayari.

 "Naomba COP28  hii ithibitike kuwa hatua ya mageuzi, inayoonyesha nia ya kisiasa iliyo wazi na inayoonekana ambayo inaweza kusababisha uharakishaji madhubuti wa mabadiliko ya kiikolojia," alisema Francis.     

Papa huyo mwenye umri wa miaka 86 pia alisema ulimwengu unapaswa kuachana na matumizi ya nishati ya visukuku. Hotuba ya Francis, ambaye alifuta safari yake ya Dubai kutokana na homa, ilisomwa na afisa wa pili wa juu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin.

Kuendeleza matumizi ya nishati ya nyuklia ? 

Nchi zinazoendelea zaomba fidia kutoka nchi tajiri zinazochafua mazingira
Nchi zinazoendelea zaomba fidia kutoka nchi tajiri zinazochafua mazingiraPicha: Chris Jackson/Getty Images

Viongozi wa mataifa yanayoendelea walijitokeza katika siku ya pili ya mkutano wa Dubai kuzishinikiza nchi tajiri zenye viwanda kuchangia ujuzi wao wa kupambana na ongezeko la joto duniani na kupunguza mizigo ya kifedha inayowakabili huku wakipiga debe maliasili zao wenyewe zinazomeza kaboni inayonasa joto hewani.

Wakati huohuo, kundi la zaidi ya mataifa 20 lilitoa wito wa kuongezwa mara tatu kwa uzalishaji wa nishati ya nyuklia inayozalishwa ulimwenguni ifikapo 2050. "Ninataka hapa kusisitiza ukweli kwamba nishati ya nyuklia ni nishati safi na inapaswa kurudiwa", alisema Emmnuel Macron rais wa Ufaransa, ambaye nchi yake inapata karibu theluthi mbili ya umeme wake kutoka kwa nguvu za nyuklia.