1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Uturuki zakubaliana kumaliza tofauti Syria

16 Februari 2018

Marekani na Uturuki zimekubalina Ijumaa kujaribu kuokoa uhusiano wao wa kimkakati, ambao Washington imekiri kuwa ulikuwa umefikia hatua ya mgogoro.

https://p.dw.com/p/2sooZ
Türkei Ankara US Außenminister Tillerson und Erdogan
Picha: picture-alliance/AA/K. Ozer

Wakati uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umetiwa doa na masuala kadhaa, Uturuki ilikasirishwa hasa na hatua ya Marekani kuliunga mkono kundi la wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria la YPG, ambalo inalichukulia kuwa la kigaidi.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari, na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, waziri wa mambo ya nje wa Marekani rex Tillerson amesema mataifa hayo mawili yana malengo sawa nchini Syria, na kuapa kuuchukulia kwa uzito, wasiwasi wa kiusalama wa Uturuki.

Katika pendekezo ambalo linaweza kuashiria hatua muhimu katika juhudi za kuondoa tofauti za washirika hao kuhusu Syria, afisa wa Uturuki alisema Uturuki imependekeza kwamba vikosi vya Uturuki na Markeani vinaweza kuwa pamona mjini Manbij.

Türkei Ankara US Außenminister Tillerson und Erdogan
Rais Reccep Tayyip Erdogan akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani rex Tillerson katika ikulu ya rais mjini Ankara, Uturuki, Februari 15, 2018.Picha: picture-alliance/AA/K. Ozer

Kuondolewa kwa YPG Manbij

Hatua kama hiyo inaweza kuchukuliwa ikiwa wapiganaji wa kundi la YPG wanajitoa kwanza na kwenda katika maeneo ya mashariki mwa Mto Euphrates, jambo ambalo Uturuki imekuwa ikilidai kwa muda mrefu.

"Tunataka kuratibu namna ya kutuliza maeneo kwa pamoja na nani atakalia maeneo hayo na malengo, nia ikiwa kurejesha vijiji hivi, miji hii kwa watu waliokuwepo kabla ya kutekwa na kundi la Daesh. Hivyo tutashughulikia kwanza Manbij. Ni mmoja ya maeneo tunayokwenda kuyafanyia kazi," alisema Tillerson.

Cavusoglu amesema Uturuki itaweza kuchukuwa hatua za pamoja na Marekani nchini Syria baada ya kundi la YPG kuondoka Manbij na maeneo ya jirani. Pia amesema mataifa hayo mawili yameanzisha mfumo kwa ajili ya mazungumzo zaidi, na watakutana tena kufikia katikati mwa mwezi Machi kuzungumza zaidi kwa lengo la kumaliza kabisaa tofauti zao.

"Laazima tuwe na uhakika wa hatua tutakazozichukuwa na laazima tuwe na uhakika kwamba YPG wanakwenda mashariki mwa Mto Euphrates. Laazima tuone utekelezaji. Ili maeneo haya yarejeshewe utulivu, suala la nani atayaongoza na kulinda usalama ni muhimu, na Rex Tillerson pia amelisema hili."

Mazungumzo hayo yalifuatia mkutano mrefu kati ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Cavusoglu na Tillerson Alhamisi usiku, ambapo masuala kadhaa ya mtafaruku yalijadiliwa.

Türkei Mevlut Cavusoglu, Rex Tillerson
Tillerson akipeana mkono na waziri mwenzake wa Uturuki Mavlut Cavusoglu, kabla ya mkutano wao mjini Ankara, Uturuki, Ijumaa Februari 16, 2018.Picha: picture-alliance/AP Photo/Anadolu

Kiini cha mzozo kati ya Marekani na Uturuki

Pamoja na Syria, masuala hayo yalihusisha malalako ya Ankara dhidi ya kiongozi wa kidini wa Uturuki anaeishi uhamishoni nchini Marekani, ambaye Erdogana anamtuhumu kwa kupanga njama ya mapinduzi iliyoshindwa mwaka 2016, wasiwasi wa Marekani kuhusu demokrasia nchini Uturuki na upinzani dhidi ya mipango ya Uturuki kununua mifumo ya kinga dhidi ya makombora kutoka Urusi.

Uturuki inakasirishwa na inachokichukulia kuwa kusita kwa Marekani kumrejesha Fethullah Guleni, na kushtakiwa nchini Marekani, kwa mtendaji wa benki wa Kituruki anaetuhumiwa kuisaidia Iran kukwepa vikwazo.

Kwa upande wake Marekani inaghadhabishwa na kufungwa kwa waandishi wa habari na wapinzani,  raia wa Marekani na wafanyakazi wa Kituruki kwenye balozi zake ndogo kwa madai ya kuhusika na ugaidi.

Ziara ya Tillerson imekuja wakati kukiwa na ongezeko la matamshi makali katika siku za karibuni dhidi ya Marekani kutoka kwa maafisa wa Uturuki, wakiwemo rais Erdogan na waziri Cavusoglu, huku rais Erdogan akisema wiki hii kuwa Wamrekani wanastahili kibao cha Ottoman, akimaanisha nguvu ya himaya ya Ottoman kwa wakati mmoja.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, Ape

Mhariri: Saumu Yusuf