Marekani, Urusi zashutumiana UN kuhusu Syria
28 Aprili 2017Majibizano hayo makali yalitokea wakati wa mkutano wa kila mwezi wa baraza la usalama kuhusu hali ya kibindamu nchini Syria. Awali balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Petr Iliichev alisema kwamba kwa ujumla, mpango wa kusitisha mapigano uliofikiwa Desemba 30 unaendelea kuheshimiwa, ingawa kulikuwepo na mienendo ya yale alioyaita makundi ya kigaidi, na matukio yanayoudhoofisha mpango huo, ambayo yanaathiri ufikishaji wa misaada.
Mkuu wa misaada ya kibidamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien aliliambia baraza kuwa hali mbaya ya kibinadamu inazidi kudorora, na kufahamisha kuwa hakuna hata msafara mmoja wa misaada umeweza kufika katika maeneo yaliozingirwa nchini Syria mwezi huu, kutokana na kukosa ruksa, hasa kutoka serikali ya rais Bashar al-Assad.
"Wakati ukosefu wa usalama unasababisha hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi kwa mamia ya maelf, njia za kuwapatia msaada unaoweza kuokoa maisha zinazuwiwa kila mara. Natiwa wasiwasi na kuongezeka, narudia -- kuongezeka, katika vikwazo vya kiutawala na ukiritimba mwingine kwa pande zote," alisema O'Brien.
Urusi ndiyo yapaswa kushinikizwa
Balozi Nikki Haley alivituhumu vikosi vya serikali ya Syria kwa kuchukulia ugavi wa dawa - kikiwemo chakula cha watoto, mashine za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo kutoka kwenye misafara ya misaada na kuviuza kwenye soko la magendo kwa bei za juu, baadhi vikiuzwa katika maeneo yanayokumbw ana mashambulizi ya mara kwa mara, na kusema hii ni biashara kubwa nchini Syria.
"Wengi wenu mmesema tunahitaji kuuwekea shinikizoutawala wa Syria. Hivyo sivyo ilivyo. Tunahitaji kuiwekea shinikizo Urusi, kwa sababu Urusi inaendelea kuulinda utawala wa Syria. Urusi inaendelea kuwaruhusu kuzuwia misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wanaoihitaji," alisema Balozi Haley.
Alisema Urusi inaendeela kumlinda kiongozi anaetumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake. Urusi inaendelea kupiga kura za turufu na Assad anaendelea kufanya yote hayo kwa sababu Urusi itaendelea kumlinda. "Hivyo nitawambia hivi, macho na shinikizo tunapaswa kuvielekeza kwa Urusi, kwa sababu wao ndiyo wanaweza kukomesha haya ikiwa watataka."
Haley, akizungumza mwisho kama rais wa baraza la usalama kwa mwezi huu, Haley alisema ataendelea kushinikiza hatua za baraza hata kama Urusi itaendelea kutumia kura ya turufu dhidi ya maazimio kuhusu Syria, kwa sababu na hapa namnukuu: Ni sauti zetu zinazopaswa kusikika, kwa sababu watu wa Syria hawajali kuhusu diplomasia.. "Wanajaribu tu kuishi siku zao za mwisho kabisaa," alisema.
Urusi nayo yawabana washirika wa waasi
Balozi wa Urusi Iliichev, akizungumza baada ya Haley akamuuliza balozi huyo wa Marekani: "Siyo wewe wala wenzako wa magharibi amesema neno lolote kuhusu mnachokofanya kuboresha hali. Unawashinikiza vipi wapinzani wenye msimamo wa wastani au wasio na msimamo wa wastani ambao una ushawishi juu yao?"
Umoja wa Mataifa unatumai kuzikutanisha serikali ya Syria na upinzani mjini Geneva mwezi ujao kwa ajili ya duru mpya ya mazungumzo yenye lengo la kumaliza vita licha ya ukweli kwamba ni hatua kiduchu zilipigwa katika mazungumzuo yaliopita. Zaidi ya watu 320,000 wameuawa katika vita vya Syria, ambavyo vimezivuta Urusi na Iran kwa upande wa serikali, huku Uturuki, mataifa ya Magharibi na mataifa ya Ghuba wakiunga mkono upinzani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe,rtre
Mhariri: Caro Robi