Marekani, Urusi zapiga hatua kuhusu amani ya Syria
27 Agosti 2016Akizungumza katika hoteli yalimofanyika mazungumzo hayo ya zaidi ya saa 12, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema, ''Leo tumebainisha mambo muhimu, yanayohitajika kusonga mbele katika kusimamisha mapigano.''
Kwa muda fulani, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura alishiriki katika mazungumzo hayo.
Aidha, Kerry ameongeza kuwa vikwazo vikubwa vya kiufundi kuelekea usitishwaji huo wa mapigano vimekwishaondolewa, ingawa vipo vingine ambavyo havijapatiwa ufumbuzi.
Mwenzake wa Urusi, Sergeiu Lavrov ameafikiana naye, na kuwaambia waandishi wa habari kuwa muhimu sana imepigwa kuelekea usitishaji wa ghasia nchini Syria.
Majadiliano kuendelezwa na wataalamu
Yamekuwepo matumaini ya tangazo la kuhakikisha mwisho wa vita ambavyo vimeisambaratisha Syria, au kuhusu mkondo mpya wa mazungumzo ya amani yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
John Kerry amefafanua kuwa wataalamu wa Marekani na wa Urusi wataendelea na mazungumzo mjini Geneva nasmo siku zijazo, kutafuta muafaka juu ya masuala yanayosalia, katika juhudi za kupata makubaliano ya kudumu.
Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amesisitiza kuwa pande zote hazitaki kutangaza makubaliano ya pupa, ambayo baadaye yatasambaratika.
Je, mara hii makubaliano yatadumu?
Makubaliano ya awali ambayo yalifikiwa mwanzoni mwa mwaka huu yamekwama, na John Kerry amesema ukikaji wa makubaliano hayo umekuwa ni kitu cha kawaida kabisa.
Marekani na Urusi zinaunga mkono kambi zinazokinzana katika mzozo wa Syria, ambao ulianza mwaka 2011 baada ya serikali ya Rais Bashar al- Assad kuyakandamiza mandamano ya wanaharakati wa demokrasia.
Urusi ni mshirika muhimu wa serikali ya Rais Assad, wakati Marekani ikiuunga mkono Muungano Mkuu wa Upinzani pamoja na makundi kadhaa mengine ya waasi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Kerry, yapo mambo mawili muhimu yenye kipaumbele, kuhakikisha usitishaji mpya wa mapigano unafanikiwa; la kwanza ni kuishinikiza serikali ya Syrika isikiuke makubaliano hayo, na la pili, ni kudhibiti ushawishi unaozidi kuongezeka wa kundi la Al-Nusra Front.
Kundi hilo limejipa jina jipya la Fateh al-Sham Front, baada ya kujitenga na mtandao wa al-Qaida. Hata hivyo, John Kerry amesema kubadilisha jina kwa kundi hilo hakutayafunika malengo halisi ya kundi hilo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre
Mhariri: Sudi Mnette