Marekani: Tutaisaidia Msumbiji kupambana na uasi
9 Desemba 2020Vyanzo vya kijeshi vimeliambia shirika la habari la AFP kuwa mapema wiki hii, wapiganaji wa kundi hilo la kijihadi linalojulikana kama Ahlu Sunna Wa-Jamaa walishambulia kijiji kimoja kaskazini mwa Msumbiji karibu na sehemu kunakoendeshwa mradi mkubwa wa gesi.
Marekani imesema waasi hao wana mafungamano na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu, na imeahidi kuisaidia serikali ya Msumbiji kukabiliana na kundi hilo.
Soma zaidi: Wanajeshi wa Msumbiji kupambana na waasi
Wapiganaji hao wanaoendesha harakati zao za uasi katika mkoa wa Cabo Delgado, mkoa wenye utajiri wa mafuta na kunakofanywa miradi ya kuchimba gesi yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 60, wameanza kupanua harakati zao za uasi.
Athari za uasi zimeshuhudiwa pia katika nchi jirani ya Tanzania, inayopakana na Msumbiji na kusababisha nchi hizo mbili kuanzisha oparesheni ya pamoja ya kijeshi kukabiliana na wapiganaji hao.
Marekani itaisaidia Msumbiji na mbinu za kijasusi
Mratibu wa kukabiliana na ugaidi nchini Marekani Nathan Sales, alipofanya ziara nchini humo na Afrika Kusini amewaambia wanahabari kwa njia ya simu kuwa Marekani inataka kuwa mshirika wa usalama wa Msumbiji ili kukabiliana na athari zozote za kiusalama.
Sales amesema Marekani inaweza kuisaidia serikali ya Msumbiji na mbinu za kijasusi, na pia jinsi ya kujibu mashambulizi.
Kauli ya Sales inaonyesha picha kamili juu ya mtazamo wa Marekani kuhusu mzozo unaoendelea kutokota nchini Msumbiji.
Mratibu huyo wa kukabiliana na ugaidi amesema Afrika Kusini ina jukumu muhimu kama nchi yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na demokrasia dhabiti barani Afrika, akionyesha matumaini kuwa nchi hiyo itajiunga na juhudi za Marekani kuutokomeza kabisa uasi nchini Msumbiji.
Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani inaonekana kuhamisha vipau mbele vyake vya kupambana na ugaidi na badala yake inaonekana kuweka juhudi kubwa za kupunguza ushawishi wa China na Urusi katika bara la Afrika na sehemu nyengine duniani.
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu linalofahamika kama Ahlu Sunna Wa-Jamaa lilitangaza ushirika wake na kundi linalojiita Dola la Kiislamu mnamo mwaka 2019, lakini uhalisia wa ushirika wao ulikuwa bado hauko wazi.